Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar  Khamis Abdulla Said  akijadili jambo  na Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar  Dkt. Mzuri Issa katika kongamano la kujadili nafasi ya mwawake katika ngazi zamaamuzi lilifanyika Ukumbi wa Dkt.Shein ZURA Mjini Unguja  .  

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Zanzibar  Khamis Abdulla akijadili jambo  na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Tone Tinnes katika kongamano la kujadili nafasi ya mwawake na uongozi  lilifanyika Ukumbi wa Dkt.Shein ZURA Mjini Unguja  .  

Mjumbe wa Mkutano Mkuu UVCCM Mkoa wa Mjini  Zainab Saleh Salim akichangia katika kongamano la kujadili nafasi ya mwawake na uongozi  lilifanyika Ukumbi wa Dkt.Shein ZURA Mjini Unguja  .  

PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO ZANZIBAR .

……..

Na Fauzia Mussa,       Maelezo Zanzibar

Serikali zote mbili zitendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika   kutekeleza mikakati maalum ya  kuwawezesha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi ili kuweka usawa wa kijinsia.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  wakati wa kongamano  la kujadili nafasi ya mwanamke na  uongozi naibu wa Wizara hiyo Anna Athanas Paul amesema kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi inaonyesha wazi juhudi zinazochukuliwa  na Saerikali hizo pamoja na  kudumisha ,demokrasia Nchini.

Amesema nafasi zinazotolewa kwa wanawake si kwa upendeleo bali ni kwaajili ya kuziba mapengo yaliyoletwa na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia pamoja na kwenda sambamba na mifumo ya kuwandaa wanawake kuweza  kuingia katika vyombo vya maamuzi.

Amesema historia inaonesha kuwa wanawake wengi  waliachwa nyuma kutokana na mila na desturi zilizokua zikikandamiza haki zao hadi pale ilipotiliwa mkazo kitaifa na kimataifa  na  kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika vyombo hivyo.

Amesema adhma ya kufikia usawa wa kijinsia ni agenda inayotiliwa mkazo kimataifa hivyo aliwaomba wadau wa maswala hayo kuendeleza jitihada zao na  kwenda sambamba na mifumo maalum ya   kuwaendeleza  wanawake ikiwa   ni utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa   ili kuwawezesha wanawake  kujitambua na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa katika  Adhma hiyo.

Aidha aliwashukuru TAMWA ,PEGAO na  ZAFELA kwa kutekeleza vyema mradi wa kuwawezesha wanawake  kushika nafasi za uongozi (SWIL) kwa ufadhili wa  Norway  unaoendelea kutoa  mafunzo kwa wanawake  Unguja na Pemba ili kuwawezesha kugombania nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali vya kisiasa.

Hata hivyo aliwataka wanawake hao kuzitumia vyema  fursa za kuchagua na kuchaguliwa ili kupata haki yao ya kushiriki katika ngazi za maamuzi na kuleta maendeleo Nchini.

Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar  Khamis Abdulla Said alisema ipo  haja kwa taasisi za Serikali na binafsi kuhakikisha kunakuwa na  uwiano mzuri kati ya wanawake na wanaume katika  upatikanaji wa fursa mbalimbali za maenedeleo

Amesema wizara ya elimu  ni  miongoni mwa wadau wanaunga mkono juhudi za kupinga vitendo vya udhalilishaji kwani wameliweka  suala la jinsia katika mitaala ya elimu na kubainisha kuwa  wizara hiyo ni yakupigiwa mfano kwa kuweka usawa katika ugawaji wa nafasi za uongozi.

Aidha alifahamisha kuwa  wizara hiyo  inaendeleza  jukumu la kuwawezesha wasichana kujitambua tangu msingi  kupitia masomo mbalimbali ikiwemo ya uongozi  maskulini.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari (TAMWA)  Pemba Fat-hiya Said maesema kupitia  mradi wa SWILL,wanawake wengi wameweza kujitokeza katika kugombania nafasi za uongozi ili kutimiza haki zao za kidemokrasia .

Amesema Dini ya Kiislamu   haimzuwii  mwanamke kushiriki katika masuala ya uongozi na  vyombo vya maamuzi hivyo amewaomba kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili  kuweza kupata haki yao ya kuchaguwa na kuchaguliwa.

Akizungumza kwa  niaba ya washiriki wa kongamano hilo   Mjumbe wa Mkutano Mkuu UVCCM Mkoa wa Mjini  Zainab Saleh Salim alisema matarajio yao   ni kuongeza  muamko kwa wanawake kuweza  kupambania kushika nafasi  mbalimbali za uongozi.

Kongamano hilo la  siku moja limefanyika katika  siku 16 za harakati za kupinga vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto likiwa na  kauli mbiu “ungana wekeza kuzuia ukatili  dhidi ya wanawake na watoto.”