Na Timothy – Mwakyenda – MAELEZO.

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika Jimbo la Newala Vijijini mkoani Mtwara kwa kutenga fedha za matengenezo na kutoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha barabara zilizoharibiwa na mvua zinakarabatiwa kwa haraka ili kurejesha mawasiliano na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa bungeni – Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Newala Vijijini, Dkt. Yahaya Ismail Nawanda, ambaye alitaka kufahamu ni lini Serikali itajenga Barabara ya Mkoma One–Mnyambe–Miyuyu inayotegemewa na wananchi wa eneo hilo.

Dkt. Dugange amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa matengenezo na uboreshaji wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 37, ambayo ina umuhimu mkubwa katika kuwaunganisha wananchi na huduma muhimu za kijamii, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Ndanda.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitumia shilingi milioni 34.7 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida katika maeneo korofi ya barabara hiyo. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga shilingi milioni 59 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, matengenezo maalum pamoja na ujenzi wa kalvati moja.

“Serikali pia imepanga katika mwaka wa fedha 2028/2029 kujenga kilomita moja ya barabara hiyo kwa kiwango cha lami pamoja na kalvati kubwa katika eneo la Mto Mambi kwa gharama ya shilingi milioni 500 kupitia Mfuko wa Jimbo,” amesema Dkt. Dugange.

Katika maswali ya nyongeza, Mbunge Nawanda amehoji kuhusu mpango wa Serikali wa kuiboresha Barabara ya Nandimba–Chikundi ili iweze kupitika mwaka mzima pamoja na kufunguliwa kwa Barabara ya Nakahako–Mkululu kwa lengo la kurahisisha biashara na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Akijibu hoja hizo, Dkt. Dugange amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizo katika kuunganisha vijiji na kata mbalimbali, na tayari imetoa maelekezo kwa Mameneja wa TARURA katika mikoa na wilaya zote nchini kufanya tathmini ya barabara zilizoharibiwa na mvua na kuanza matengenezo mara moja.

“Barabara hizi ni muhimu kwa sababu zinaunganisha vijiji na kata mbalimbali. Serikali imeshatoa maelekezo kwa Mameneja wa TARURA kufanya tathmini ya maeneo yaliyoathirika na mvua na kuanza matengenezo mapema iwezekanavyo kuanzia mwishoni mwa mwezi Juni hadi mwanzoni mwa Julai mwaka huu wa fedha,” amesema.

Dkt. Dugange amemhakikishia Mbunge huyo kuwa barabara za Nandimba–Chikundi na Nakahako–Mkululu zitafanyiwa matengenezo ili kurejesha mawasiliano, kuboresha usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Sambamba na hilo, amemwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Mtwara pamoja na Meneja wa TARURA Wilaya ya Newala kufika katika maeneo husika kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina na kuanza ukarabati wa maeneo korofi, huku mipango ya matengenezo ya kudumu ikitarajiwa kujumuishwa katika bajeti zijazo.

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, pamoja na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Newala Vijijini.