Naibu Waziri wa Ujenzi,Mhandis Godfrey Kasekenya, akizungumza jambo katika hafla ya ugawaji wa Tuzo za Ujenzi na Majengo Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 (EABC), zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (katikati), akifuatilia ugawaji wa Tuzo za Ujenzi na Majengo Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 (EABC), zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia ugawaji wa Tuzo za Ujenzi na Majengo Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 (EABC), zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi,Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali itaendelea kuwaamini Wakandarasi wa Ndani kwa Miradi Mbalimbali ikiwemo ile mikubwa ambayo wanaweza wakafanya vizuri kwani Serikali tayari imeongeza wigo mpana katika sheria ya manunuzi kwa lengo la kuwanufaisha Wazawa.
Hayo ameyasema wakati wa Ugawaji wa Tuzo za Ujenzi na Majengo Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 (EABC), zilizofanyika Katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Kasekenya amesema wahandisi wanapaswa wapate vifaa bora ikiwemo Saruji, nondo, misumari, vigae, marumaru na bidhaa zote zinazotumika kwenye ujenzi ambazo zinazalishwa na kampuni hizo.
“Ukiwa mhandisi mzuri halafu ukapata bidhaa zisizobora basi hautafanya chochote kizuri. Moja ya kitu ambacho Serikali tunakitaka ni kuwa na vifaa na uhandisi bora hivyo tunatoa wito kwa wadau wanaojihusisha eneo hili kutoa huduma zilizobora ambazo zinaingia kwenye mnyororo mzima wa ujenzi”, amesema Mhandisi Kasekenya
Hata hivyo Mhandisi Kasekenya ametoa rai kwa Watanzania kuzidi kuwatumia wataalamu wa ujenzi pindi wanapokuwa na miradi ili kuwa na uhakiki na usalama wa miradi yao kumalizika kwa wakati na kuwa bora.
“Usipowatumia wataalamu ujue mbele ya safari inawezekana ukapata hasara. Kama unajenga nyumba hakikisha imesanifiwa na mtaalamu hata asipojenga yeye hakikisha anakupa ushauri”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Tuzo za Ujenzi na Majengo za Afrika Mashariki kwa Mwaka 2023 umeshindanisha makampuni zaidi ya 500 kwa lengo la kuongeza ushindani miongoni mwa wadau wa Sekta ya Ujenzi, lakini pia kufanya chachu ya utoaji wa huduma bora katika mnyororo mzima wa Sekta ya Ujenzi.