Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa,Sensa ya Filamu na Utamaduni BASFU Dkt.Omar Abdalla Adam akipata maelezo kuhusia na maonesho ya tatu ya sanaa ya uchoraji wa picha yenye mada ya “Hadithi ya bibi” kutoka kwa Lisenka Beetstra Mjumbe wa bodi ya Taasisi ya Emerson’s Foundation huko nyumba ya sanaa Hurumzi Mjini Unguja.
Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa,Sensa ya Filamu na utamaduni BASFU Dkt.Omar Abdalla Adam akizungumza na wasanii walioshiriki kugombania tunzo ya sanaa ya picha za kuchora inayojuulikana kama “Hadithi ya bibi” wakati akizundua maonesha ya sanaa hizo huko nyumba ya sanaa Hurumzi Mjini Unguja.
Baadhi ya Watalii wakitembelea maonesho ya sanaa ya picha za kuchora baada ya kuzinduliwa na Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa,Sensa ya Filamu na Utamaduni BASFU Dkt.Omar Abdalla Adam huko nyumba ya sanaa Emerson’s Foundation Hurumzi Mjini Unguja.
Baadhi ya Vijana wa Zanzibar wakitembelea maonesho ya sanaa ya Picha za kuchora baada ya kuzinduliwa na Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa,Sensa ya Filamu na Utamaduni BASFU Dkt.Omar Abdalla Adam nyumba ya sanaa Hurumzi Mjini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Muss-Maelezo
WAKFU wa Emerson Zanzibar umezindua maonesho ya picha za kuchora zilizoingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya mchoraji bora wa mwaka 2023.
Akizungumza baada ya kuzindua maonesho hayo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar (BASFU) Dkt. Omar Abdalla Adam amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafarijika kuona wadau wa sanaa wanaanzisha matukio mbalimbali yanayolenga kuibua na kukuza vipaji vya wasanii.
Alisema Maonesho na tuzo kama hizo zinazobuniwa na Taasisi binafsi, ni njia moja ya kukuza vipaji na kuwaletea tija wasanii kwa kuuza kazi zao ndani na nje ya Nchi pamoja na kuinua uelewa wa wasanii wenye tafsiri inayounganisha kizazi kipya na historia ya zamani katika malezi na maadili ya Kizanzibari.
“Zanzibar tuna utajiri mkubwa wa vitu vya historia vinavyohitaji kuchorwa ili visipotee, kwa mfano baibui la kamba lenye aina nyingi za uvaaji na maana zake hakuna kazi mbaya ya sanaa, bali tafauti ipo katika ubunifu na ujumbe unaopatikana.”Alifahamisha Katibu huyo
Katika kuthamini juhudi za Wasanii hao Katibu huyo aliahidi kuwapatia vyeti vya usajili vitakavyowawezesha kutambuliwa rasmi na BASFU kuwa ni wasanii halali bila ya malipo ili kuweza kupata haki zao nyengine ndani na nje ya Nchi.
“kwa kawaida cheti hicho kinalipiwa shiligi laki moja na nusu lakini nyinyi tutawapatia bure kabisa kama mchango wa Serikali katika kuibua vipaji vya vijana”Alieleza Katibu huyo
Awali aliwapongeza wachoraji ambao kazi zao zimeteuliwa kuwania tuzo hiyo, zinaonesha hazina ya vipaji vilivyopo nchini na kuwataka waliokosa nafasi ya kushiriki wasivunjike moyo na kujaribu katika mkupuo mwengine wa mashindano hayo.
Mratibu wa Wakfu wa Emerson Salma Adim amesema Taasisi hiyo imekuwa ikiandaa tuzo mbalimbali kwa wasanii wa filamu, muziki na picha za kuchora, kwa ajili ya kuibua na kustawisha vipaji vyao pamoja na kuitangaza Zanzibar kimataifa.
Alifahamisha kuwa mbali na uangalizi na uamuzi wa majaji, wadau mbalimbali waliohudhuria ufunguzi huo na watakaotembelea maonesho hayo watapata fursa ya kuchagua picha walizoona zinastahiki kupatiwa tuzo hiyo.
Alisema Maonesho ya picha hizo yataendelea hadi Disemba 7 na kutangazwa mshindi ifikapo Disemba 8, 2023 ambae atakabidhiwa cheti, tuzo (Trophy) pamoja na fedha taslim kiasi cha shilingi milioni mbili za Kitanzania.
Kwa upande wa Mshindi wa pili alisema atapatiwa nafasi ya kuonesha kazi zake katika nyumba hiyo na kuuzwa kwa watakaohitaji.
Maonesho hayo ni ya tatu kufanyika tangu kuanzishwa katika nyumba ya sanaa ya Emerson Hurumzi mjini Zanzibar yakibeba ujumbe“Hadithi ya Bibi” na kushirikisha wachoraji wazawa wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35.