*Kigamboni na Pangani*
Imeelezwa kuwa, zoezi la kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi wa Uchimbaji Madini Tembo (heavy mineral sands) utakaotekelezwa eneo la Fungoni Kigamboni Mkoani Dar es Salaam limefikia asilimia 92 huku kiasi cha shilingi bilioni 18 kikiwa tayari kimekwishakulipwa.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali alipotembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki kwa lengo la kuangalia hatua za uendeleaji wa mradi huo ikiwemo kujua changamoto zinazokabili utekelezaji wake ambapo alihimiza zoezi la ulipaji fidia kukamilishwa haraka ili mradi uanze kama ulivyokusudiwa.
Mradi huo unamilikiwa na kampuni ya Nyati Mineral Sand Limited ambayo ni kampuni ya ubia kati ya Serikali inayomiliki asilimia 16 ya hisa na kampuni ya Strandline Resources Limited inayomiliki asilimia 84 ya hisa unatarajia kuanza shughuli za uchimbaji madini hayo mara zoezi la kulipa fidia wananchi wanaotakiwa kupisha mradi huo utakapokamilika.
Katika taarifa iliyotolewa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu, ilielezwa kuwa kulingana na utafiti uliofanywa, mradi wa uchimbaji madini tembo una kiasi cha tani milioni 12 za mbale na uhai wa mradi ni miaka 6 kwa kuchakata tani milioni 2 za mbale kwa mwaka na kuelezwa kuwa, uchorongaji zaidi utafanyika katika maeneo hayo ili kuongeza kiasi cha mashapo na hivyo kuongeza uhai wa mgodi.
Katika hatua nyingine, Desemba 2, 2023, Katibu Mkuu Mahimbali alitembelea katika mradi mwingine wa uchimbaji madini tembo unaomilikiwa na kampuni hiyo katika eneo linalojulikana kama Tajiri Wilayani Pangani Mkoa wa Tanga ili kuangalia maendeleo ya mradi pamoja na kufahamu changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mradi husika.
Kadhalika, mradi huo, Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa na Kampuni ya Stradline Resources Limited inamiliki hisa asilimia 84.
Katika ziara hiyo ilielezwa kuwa, kulingana na utafiti uliofanywa katika eneo hilo, kiasi cha mashapo yenye kiasi cha tani milioni 268 katika ubora wa asilimia 3.3 kimegunduliwa na uhai wa mradi huo unatarajia kuwa miaka takribani 23.
Aidha, kulingana na taarifa za Wizara ya Madini, kampuni ya Nyati Mineral Sand Limited imeomba leseni kubwa ya uchimbaji madini (Special Mining Licence) na mchakato wa kutolewa leseni hiyo unaendelea. Vilevile, imeelezwa kuwa, utaratibu wa kulipa fidia wananchi watakaoathirika na mradi katika eneo hilo la pangani utafanyika mara leseni ya uchimbaji madini itakapotolewa na mara baada ya zoezi la kulipa fidia kukamilika shughuli za uchimbaji madini tembo kwenye mradi huo zitaanza.
Kampuni ya Strandline ni miongoni mwa kampuni 4 za uchimbaji wa madini ambazo mnamo Desemba 13, 2021 Serikali na kampuni husika zilitia saini makubaliano ya mikataba ikiwa ni matokeo ya marekebisho ya Sheria ya Madini ambayo ilipelekea kuipa nguvu Serikali kumiliki rasilimali hizo kwa niaba ya wananchi kwa lengo la kuleta manufaa zaidi kwa watanzania.
Kampuni nyingine zilizoweka saini mikataba ya makubaliano kipindi husika ni pamoja Black Rock Mining Limited itakayochimba madini ya kinywe wilayani Mahenge mkoani Morogoro, Nyanzaga Mining Limited itakayochimba madini ya dhahabu wilayani Sengerema mkoani Mwanza na kampuni ya Petra Diamond Ltd inayochimba madini ya Almasi Mkoani Shinyanga ambapo katika makubaliano hayo Serikali iliongeza umiliki wa hisa katika mgodi huo kutoka asilimia 25 kufikia asilimia 37.
Hafla ya utiaji saini mikataba hiyo ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu ambaye katika hotuba yake alisisitiza kuhusu shughuli za uongezaji thamani madini hayo kufanyika nchini ili kuleta manufaa zaidi kwa taifa.
Miradi ya madini tembo inatarajia kuinufaisha nchi kiuchumi ikiwa ikiwa ni pamoja na Serikali kupata mapato yatokanayo na kodi, mrabaha, ada ya ukaguzi, ushuru wa huduma na malipo mengine yanayotakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria za nchi, ikiwemo fursa za ajira kwa watanzania wakiwemo wanaozunguka eneo la mradi pamoja na ajira kupitia shughuli za utoaji huduma mbalimbali katika migodi hiyo.
Madini tembo yatakayochimbwa katika miradi hiyo ni pamoja na rutile, ilmenite, zircon na monazite. Madini hayo yana matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengeneza vioo, rangi mbalimbali hususan za magari, kutengeneza ceramics (kauri) na pia hutumika katika kinu cha nyuklia.