Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, akieleza kuhusu umuhimu wa maoni ya wadau katika uboreshaji wa Sera za Kodi wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Mtwara, ikiwa ni mwendelezo wa makongamano hayo ya uboreshaji wa Kodi.
Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, akieleza lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kutatua malalamiko ya Kodi, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Mtwara.
Mkurugenzi wa Bambo General Store Ltd, Bw. Cosmas Bambo, akitoa maoni kuhusu maboresho ya Kodi kwa mwaka 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Mtwara.
Afisa Biashara Mkoa wa Mtwara, Bi. Osmunda Kapinga (kushoto) na Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mtwara, wakisikiliza maoni ya wananchi wa mkoa huo wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda, lililofanyika mkoani Mtwara.
Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mtwara, Bw. Seleman Kadeghe, akitoa maoni kuhusu maboresho ya kodi kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, wakati wa Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Mtwara.
Baadhi ya Wafanyabiashara wakiwa katika Kongamano la kukusanya maoni ya Kodi Kikanda lililofanyika mkoani Mtwara linalohusu ukusanyaji wa maoni ya maboresho ya kodi kwa mwaka 2024/25.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mtwara)
Na. Peter Haule, WF, Mtwara
Serikali imewataka wafanyabiashara wazawa kujiunga na Mfumo Mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi ya Umma (NeST) ili kupata Zabuni zinazotolewa na Serikali na kunufaika kwa kukuza pato la mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, wakati wa Kongamano la ukusanyaji maoni ya Kodi Kikanda Mkoani Mtwara, ikiwa ni muendelezo wa makongamano kama hayo yanayofanyika Kanda mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha Sera ya Kodi kwa mwaka 2024/25.
“Mfumo wa NeST ni rafiki na shirikishi katika matumizi yake hivyo nawaomba wafanyabiashara kushiriki katika zabuni mbalimbali za Serikali ikiwa ni mwelekeo wa Serikali wa kuwapa kipaumbele wazawa ili fedha za walipa kodi zibaki ndani ya nchi kuweza kuchochea maendeleo ikilinganishwa na awali ambapo fedha nyingi zilikuwa zinawanufaisha wageni kwa kiwango kikubwa’’, alieleza Bw. Mhoja.
Aidha, alieleza kuwa kuna changamoto ambazo nchi imekutana nazo ikiwa ni pamoja na Uviko 19 lakini pia Vita ya Ukraine na Urusi ambazo zimesababisha baadhi ya bidhaa upatikanaji wake uwe changamoto lakini wafanyabiashara wanaweza kuitumia hali hiyo kama fursa ya kuongeza uzalishaji na kumiliki soko la bidhaa.
Bw. Mhoja alisema kuwa ni vema wananchi wakaongeza uzalishaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa nchini ambazo kwa sasa zina soko.
Pia alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hssan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika uwekezaji hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili iweze kukuza uchumi wa nchi.
Bw. Mhoja alisema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ya usafirishaji na Nishati, kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla na kuwa na sera za kodi zinazotabirika na kuwianisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti.
Kwa upande wake Meneja Huduma wa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Godwin Barongo, alisema kuwa, Taasisi hiyo imeanzishwa ili kutafuta suluhisho ya malalamiko ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na Mamlaka ya Mapato.
Alisema kuwa kama kuna mlipakodi ana malalamiko anayo nafasi ya kwenda kwenye Ofisi za Taasisi hiyo ambazo zipo Dodoma au kuwasiliana kwa njia ya simu ili kutatua changamoto ya mteja kwa muda mfupi na kusaidia kodi ya Serikali kulipwa bila malalamiko.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), mkoa wa Mtwara, Bw. Kizito Galinoma, alisema hatua ya Serikali kuwafikia katika Kanda zao inadhihirisha dhamira njema ya kutatua changamoto za kikodi kwa wafanyabiashara, wenye viwanda, wakulima na wavuvi, hivyo Chama hicho kitaendelea kutoa ushirikiano ili kutatua kero mbalimbali.
Timu ya Wataalam wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha ianendelea na ukusanyaji wa maoni kwa wananchi Kikanda ambapo hadi sasa Kanda tano zimefikiwa kupitia zoezi hilo lililofanyika mkoa wa Arusha, Mwanza, Kigoma, Mbeya na Mtwara.