Adeladius Makwega-MWANZA
Serikali ya Tanzania Disemba 2, 2023 imemkabidhi eneo la ujenzi wa Akademi ya Taifa ya Michezo-(National Sport Academy) Kampuni ya CRJE ili kuanza ujenzi huo mara moja inayojengwa kando ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, kilichopo Kwimba mkoani Mwanza.
Akizungumza kandoni mwa makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Manadeleo ya Michezo nchini, Ali Mayay Tembele amesema kuwa kampuni hiyo imekabidhiwa eneo hilo na ndani ya siku 14 iwe vifaa vimefika na ujenzi umeanza na ujenzi huu ni wa awamu mbili , awamu ya kwanza miezi 12, awamu ya pili miezi sita na ujenzi mzima ukiwa wa miezi 18, ukitarajiwa kukamilika kabla ya Julai 2025.
“Kituo hiki kitakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali, kama vile mpira wa miguu , netiboli ,mpira wa mikono , mpira kikapu, mpira wa wavu na bwana kuogelea lenye hadhi ya Olmpiki. Hatua ya kwanza watajenga viwanja ya michezo na hatua ya pili ni mabweni .Gharama zote ya mradi huu ni bilioni 31 zikigharamia na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Akizungumza katika kikao cha utangulizi kabla ya makabidhiano ya eneo la mradi huu, Mkurugenzi Tembele alisema kuwa yupo hapa Malya kumuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndugu Gerson Msigwa na kuiwakilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoboresha michezo na kuwathamini wadau wote wa michezo nchini.
“Nimefika mbele yenu kifua mbele, sasa michezo inapiga hatua zake kwa kasi kubwa, nawaomba kampuni ya CRJE ifanye kazi vizuri na serikali itatoa ushirikiano wote unaohitajika kama makubaliano yalivyo katika mkataba. Kama makubaliano yalikuwa milango iwekwe ya Mninga basi iwekwe milango ya Mninga na siyo mbao nyingine na kinyume chake ni kuichokoza serikali ”
Mkurugenzi Ali Mayay pia amewaomba wananchi wa Malya wajitahidi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa mradi huo maana mradi huu ni mali yao .
“Sisi ni watumishi wenu ndugu zangu wananchi, lindeni mradi wenu.”
Akijibu hoja ya kutoa ushirikiano huo kandoni ya makabidhiano hayo Diwani wa Kata ya Malya wilaya Kwimba mkoani Mwanza Atanasi Migo Mayunga ambaye ndiye kiongozi wa kisiasa aliyeshuhudia zoezi hilo alisema kuwa ushirikiano utatolewa bila shida yoyote maana mradi huo unakuja kuifufua kata yake upya,
“Nakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa mradi huu, kwa sasa kata yangu inamradi wa bilioni 31, ambapo awali ilikuwa kama ndoto ya mchana kumbe ni kweli.”
Akizungumza wakati wa utangulizi katika shughuli hii Richard Mganga, Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya amesema kuwa ujio wa kituo hicho ni muhimu katika programu zima ya kuendeleza michezo Tanzania,
“Kituo hichi ni muhimu sana kitatoa nafasi ya kupata wachezaji mahiri na kitakuwa mahali pa kuwapika wachezaji kadhaa wa kitaifa na kimataifa.”
Shughuli hiyo iliambatana na shamrashamra za ngoma za kimakabila kutoka kwa wanachuo wa chuo hiki.
“Kuanza kwa ujenzi huo ni mwanga mpya kwa sekta ya michezo nchini Tanzania .”
Hayo yakisemwa na Kasili Lameck, Waziri wa Michezo wa Serikali ya Wanachuo Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya CRJE ndugu Wang Dong alisema,
“Tunashukuru sana kukabidhiwa eneo hili la mradi, tunafanya maandalizi yote na kazi hii tutaifanya vizuri, msiwe na shaka yoyote.”
Naye Msanifu Majengo kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi na Mkandarasi Mshauri Peter Mahimbo amesema kuwa anafuraha mradi huo kukabidhiwa kwa mkandarasi CRJE
“Tunatarajia kusimamia mradi huu vizuri maana mkandarasi huyu ni bora, anafanya kazi vizuri, hapa Tanzania amefanya kazi nyingi za kupigiwa mfano.Sisi tutatimiza wajibu wetu”
Katika zoezi hilo serikali imesema bayana kuwa sasa miradi mikubwa kama hii itaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali lakini kikubwa lazima kila halmashauri ziyatunze maeneo yao ya viwanja vya michezo.