Benki Kuu ya Tanzania imebaini uwepo wa taasisi, kampuni na watu binafsi wanaojitangaza kuwa mawakala au washauri elekezi (consultants) wanaotoa huduma ya kusaidia waombaji kupata leseni au usajili wa watoa huduma ndogo za fedha, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, benki na taasisi za fedha, watoa huduma za mifumo ya malipo, na watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zinazosimamiwa na Benki Kuu. Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutarifu umma kwamba haina utaratibu wa kuwataka waombaji wa leseni au usajili wowote kutumia washauri kwenye uandaaji na uwasilishaji wa maombi ya leseni.
Aidha, Benki Kuu imebaini kuwa baadhi ya matangazo yanayotolewa na washauri sio sahihi hasa gharama zinazohusika. Hivyo Benki Kuu inawataka washauri hao watenganishe gharama za huduma za ushauri na zile za leseni za Benki Kuu kwenye matangazo yao. Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015 na kanuni zake zimeainisha viwango vya mitaji na gharama za maombi ya leseni ya kila aina ya taasisi. Gharama ya maombi ya leseni, ambazo hulipwa moja kwa moja katika akaunti ya Benki Kuu, ni kama zilivyoainishwa katika jedwali:
Na. | Aina ya Taasisi | Ada ya Maombi ya Leseni (Shilingi) | Ada ya Leseni (Shilingi) |
1. | Benki na Taasisi za Fedha | Milioni Kumi | Hakuna |
2. | Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni | Milioni Moja | Laki Tano kwa Mwaka kwa kila Tawi |
3. | Watoa Huduma Ndogo za Fedha (Mtu binafsi) | Laki Tatu | Hakuna |
Na. | Aina ya Taasisi | Ada ya Maombi ya Leseni (Shilingi) | Ada ya Leseni (Shilingi) |
4. | Watoa huduma ndogo za fedha (Kampuni) | Laki Tano | Hakuna |
5. | Watoa huduma za mifumo ya malipo | Milioni Moja | Milioni Kumi na Mbili kwa Miaka Mitano |
6. | Watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu | Milioni Moja | Milioni Mbili kwa Miaka Mitano |
Benki Kuu ya Tanzania inawakumbusha waombaji wa leseni na umma kwa ujumla kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa katika kuandaa na kuwasilisha maombi ya leseni au usajili wa taasisi tajwa ambazo zinasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha,
Benki Kuu ya Tanzania,
2 Mtaa wa Mirambo, S.L.P 2939,
DAR ES SALAAM.
Simu Na. +255-22-223-5483
Barua Pepe: [email protected] au [email protected]