Na Mwandishi wetu, Kiteto
WAANDISHI wa habari wa Mkoa wa Manyara, wamekutana na polisi wa Wilaya ya Kiteto kwenye mdahalo wa ulinzi na usalama wa waandishi wa habari.
Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa muungano wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania, (UTPC), Musa Yusuph amesema mdahalo huo utaimarisha ushirikiano wa waandishi na polisi.
Yusuf amesema wamefanya midahalo maeneo mbalimbali nchini baina ya waandishi na polisi ambao lengo lao wote ni kuhudumia jamii.
Mkuu wa polisi Wilaya ya Kiteto, (OCD) Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP) Paul Mashimbi amesema waandishi na polisi wakikaa pamoja na kupanga watafanikisha kazi zao
“Kabda ya kwenda kazini polisi na waandishi wakikaa pamoja na kuzungumza hakuwezi kuwa na migogoro au migongano kazini kwani mtakuwa mmekutana kabla,” amesema OCD Mashimbi.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara (MNRPC) Zacharia Mtigandi amesema lengo la kufanyikia ni kuimarisha mahusiano ya polisi na waandishi wa habari Kiteto.
“Baadhi ya waandishi wa habari Kiteto walikuwa na msuguano na baadhi ya taasisi za serikali hivyo chama kikaona ni vyema kufanya mdahalo huu Kiteto kwa lengo là kuimarisha uhusiano baina yao,’ amesema Mtigandi.
Mmoja kati ya waandishi wa habari kutoka wilayani Kiteto, Mohamed Hamad amesema mdahalo huo kufanyikia Kiteto utaongeza chachu ya mshikamano kwao.
“Tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa baina yetu waandishi wa habari na polisi hivyo vikao kama hivi vikifanyika mara kwa mara vitaongeza tija na ufanisi baina yetu,” amesema Hamad.