Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, akizungumza na wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wakati wa Mahafali ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), wakishangilia baada ya kutunukiwa shahada mbalimbali na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (hayupo pichani) wakati wa Mahafali ya 49 ya Chuo hicho yaliyofanyika, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahitimu Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), wakivaa kofia kuashirikia kutunukiwa shahada mbalimbali na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (hayupo pichani) wakati wa Mahafali ya 49 ya chuo hicho yaliyofanyika, jijini Dar es Salaam.
Na Scola Malinga, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ametoa wito kwa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kuendeleza juhudi za kubuni na kuboresha mitaala ili kutoa mafunzo kwa viwango vya kimataifa kwa vijana wa kitanzania.
Ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya Arobaini na Tisa (49) ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha.
Mhe. Chande alisema mifumo ya elimu imeendelea kubadilika kutokana na mazingira yaliyopo na mabadiliko hayo hayazuiliki, kwa kuwa mambo mapya yanaibuka kila wakati.
“Ili Tanzania iweze kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda, ni lazima kuwa na mifumo bora ya elimu na hasa katika elimu ya juu. Hii ndio sababu, moja ya malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 ni kuhakikisha kuwa tunajenga jamii inayoelimika, inayojifunza na inayojenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani”, alisisitiza Mhe. Chande.
Aidha, alikipongeza Chuo hicho kwa juhudi za kubuni na kuboresha mitaala ili iweze kuendana na mahitaji ya soko la ajira, na katika kukabiliana na uhaba wa wataalamu nchini hasa katika fani za Fedha, Benki, Bima, Tehama na Hifadhi ya Jamii.
Mhe. Chande alisema uchumi wa mataifa yote duniani unategemea wataalamu wa fedha na fani nyingine zinazoendana na fedha kama Benki, Kodi, Bima, Tehama, na Hifadhi ya Jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Josephat Lotto alisema Chuo chake kinaendelea na uboreshaji wa mitaala ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko na inatoa majibu kwa vitendo kwenye matatizo ya jamii ya Kitanzania.
Alisema uboreshaji wa mitaala wakati mwingine ina sababisha kuanzishwa kwa mitaala mingine na hivyo Chuo hicho kimeanzisha Shahada ya kwanza kwenye eneo la Usalama wa Mtandao (Bachelor Degree in Cyber Security) ambayo imeanzishwa ili kusaidia wahitimu kuwa na ujuzi wa kutengeneza na kuanzisha mifumo salama ya kompyuta na mitandao, kuhakikisha inatumika kwa usalama.
Aliongeza kuwa ujuzi huo ni muhimu kwa kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuimarisha, kuboresha na kueneza mfumo wa TEHAMA nchi nzima na uinuaji wa sekta binafsi.
Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kilianzishwa mwezi Julai mwaka 1972, kikiwa na wanafunzi 72 hadi kufikia 2022/2023 kumekua na ongezeko la wanafunzi kufikia 12057 katika vyuo vyake vya Dar es Salaam, Dodoma, Simiyu na Mwanza.