Arusha .WAKALA wa Usajili wa Biashara na leseni (BRELA), imeanzisha Mkakati wa kuwahamasisha wavumbuzi wote nchini, kuzilinda kazi zao kisheria kwa kuzisajili ili kuepusha kutumiwa na watu wengine na hivyo kunufaika na bunifu hizo ikiwemo vifaa,dawa na bidhaa zingine mbalimbali.
Akizungumza jijini Arusha, Msajili Msaidizi wa BRELA, wakati akitoa elimu kwa wafanyabiashara wa jijini Arusha,Benedictson Byamanyilwowa alisema wameamua kuzunguka maeneo mbalimbali nchini, ili kutoa elimu ya Hataza (uvumbuzi) kwa wafanyabaishara kwa lengo la kutoa elimu itakayowasaidia vumbuzi kutumiwa na watu wengine.
Alisema Dunia kwa sasa inaishi kwa teknolojia na uvumbuzi, hivyo wapo baadhi ya watu wanavumbua vifaa au dawa mbalimbali vinavyotatua matatizo mengi katika jamii na kuanza kuvitumia sokoni au katika jamii bila kusajili BRELA na jasho lao kupotea bure.
“Sasa kwa kuanza kutumia sokoni au katika jamii ni kosa kubwa kisheria na ukibainika hatua zipo kali za kisheria za kukuchukulia, sasa tumeamua kuja kutoa elimu hii ni laima unapovumbua kitu chochote iwe kifaa, dawa na vingine vingi lazima uje kwetu usajili,”alisema.
Aidha alisema mtu anaposajili dawa, au kifaa chake anakilinda kisheria na kupata manufaa mengi ya kulindwa kisheria, toifauti na anapotumia bila kusajili.
“Hii inahusu hata wale wavumbuzi wa vyuo vikuu vya kati wapo wanaovumbua vifaa vyao ni lazima wote kabla hawajaanza kupeleka sokoni au katika jamii wakilete kwetu kusajili na wapo hata baadhi yao wanapeleka katika maonyesho ya Sabasaba au Nanenane kabla hawajasajili hili ni kosa,”alisema
Naye Ofisa Msajili BRELA, Julieth Kiwelu alisema wapo Arusha kutoa elimua kwa ajili ya kuongezea uwezo wafanyabiashara, ili watumie bunifu zao katika biashara zao.
“Tunawapa elimu jinsi ya kuweza kutumia bunifu zao katika biashara zao kwa kufuata sheria za nchi kupitia BRELA na tutaenda wilaya mbalimbali katika mkoa huu ili kila mmoja apate elimu hii”.
Afisa Biashara wa Chama cha Wafanyabaishara Mkoa wa Arusha,Charles Makoi alishukuru BRELA kwa kuwapatia elimu hiyo ambayo itawasaidia kufanyabiashara kwa kufuata sheria na kuepuka ufanyaji biashara kimazoea.
Pia unapovumbua au unapobuni kitu chako ni muhimu kusajili,vinginevyo mwenzako anapofahamu hujasajili, anatumia mwanya huo kwa kuja kusajili haraka BRELA na inakua haki yake, wewe unapokwenda kutaka kusajili umechelewa, matokeo yake unaanza kusumbuana na kesi miaka mingi bila mafanikio,”alisema.