Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,Abubakari Kunenge ameiagiza idara ya elimu mkoa kusimamia kikamilifu Shule Maalum ya Sekondari ya wasichana wenye vipaji ya Bibi Titi Mohammed iliyopo Utete ,Rufiji ili iwe kimbilio na mfano wa kuigwa kati ya shule kumi maalum za Sekondari za wasichana zilizojengwa nchini na Serikali.
Vilevile, amemuagiza Katibu Tawala mkoa pamoja na Ofisa elimu mkoani humo kuweka mikakati madhubuti ili shule hiyo iwe na kiwango kizuri kwenye taaluma.
Akipokea vitanda 40 vitakavyobeba watoto 80 vyenye gharama ya milioni 12 kutoka Taasisi ya kifedha ya NMB , sanjali na mabox ya maziwa kutoka kampuni ya ASAS , Kunenge alieleza Rais Samia Suluhu Hassan anaonyesha jitihada kuboresha sekta ya elimu ,haina budi kusimamia jitihada hizo .
“Rais amedhamiria kuboresha mazingira ya sekta ya elimu na tayari ameanzisha shule za Sekondari maalum za wasichana kumi ambapo nyingine 16 awamu ya pili zitajengwa nchi nzima kufikia idadi ya shule 26, pia shule za Msingi 219 na za Sekondari 718 zimejengwa ,” alifafanua Kunenge.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa , ameahidi kufanya mpango wa kupeleka mtambo wa mtungi wa gesi shuleni hapo .
Kunenge aliagiza wakala wa maji safi Mijini na Vijijini (RUWASA) wafanye utaratibu shule hiyo ipate maji ya uhakika.
Kadhalika na hilo ,Wakala wa Barabara (TANROADS) kung’oa visiki na kufanya maboresho madogomadogo katika barabara inayoelekea kwenye shule ya Bibi Titi Mohammed.
Pia Halmashauri ya wilaya ya Rufiji imetakiwa kupange Mji wa eneo hilo ili Mji ukue na shule iondokane kukaa kifichoni.
Kuhusu umeme , Kunenge alieleza mradi mkubwa wa ujenzi wa umeme unaendelea kutokea Mbagala-Mkuranga hadi Utete na mradi mwingine mkubwa wa kimkakati wa bwawa la Mwalimu Nyerere Stigo hali itakayowezesha kutatua tatizo la Umeme Utete na kuwa nishati ya umeme ya uhakika.
Awali akikabidhi vitanda hivyo ,Mkuu wa Matawi ya bank ya NMB/mauzo Donatus Richard , alieleza wametoa vitanda 40 ikiwa ni sehemu ya wanachochangia wateja wanarejesha faida kwa jamii.
Alieleza, wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya elimu na afya .
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowelle alishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule ya Sekondari Bibi Titi Mohammed ambayo imejengwa kwa gharama ya Bilioni 4.1.
Taarifa ya shule hiyo inasema ,licha ya Serikali na wadau kuongeza nguvu ya kuboresha mazingira bora ya shule , lakini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa uzio hali inayowapa hofu kutokana na wanyama wakali .
Changamoto nyingine ni , upungufu wa vitabu vya masomo ya sayansi na vifaa vya maabara, kutokuwa na maji ya uhakika wanaomba kuchimbiwa visima na kukatikakatika kwa umeme.