NA SABIHA KHAMIS MAELEZO
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa amesema tafiti za tathmini zitakazowasilishwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) zitasaidia kutumika katika kutunga mitaala mipya ili kuboresha Sekta ya Elimu Nchini.
Akizungumza wakati akifungua Kongamano la Kuadhimisha Miaka 50 ya Baraza hilo huko Skuli ya Utalii Maruhubi amesema Amesema tafiti hizo zitatoa takwimu sahihi zitakazotoa taarifa za ukweli na uhakika ambazo zitasaidia kuboresha mapungufu yaliyopo na kuleta maendeleo ya Elimu Nchini.
Waziri Leila aliwataka washiriki kulitumia kongamano hilo kwa mbinu za tathmini zinazoendana na karne ya 21.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Said Ali Mohamed amesema, lengo la Kongamano hilo ni kuiandaa Sekta ya Elimu katika kutumia Teknolojia wakati wa utahini, upimaji wa wanafunzi pamoja na kuandaa mitaala.
Amefahamisha kuwa katika kipindi cha miaka 50 wamefanikiwa kufanya tathimini ya walipotoka na walipo na kuahidi kutatua changamoto zitakazojitokeza ili kuweza kujiandaa kutoa mitaala itakayokwenda na wakati.
Aidha, amesema kongamano hilo litasaidia kuratibu na kufanya mitihani ya Watu wenye mahitaji maalum pamoja na kuweka ushirika wa Mtandao ambao utaendeleza Sekta ya Elimu na kuikuza heshima ya Nchi.
kongamano hilo la siku mbili limewashirikisha wataalamu kutoka Vyuo Vikuu vya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Nchi jirani ikiwemo Kenya na Uganda kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano uliopo.