WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ,akielezea jambo wakati wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Madini ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde akizungumza katika Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga,akitoa taarifa wakati wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi.Rosemary Senyamule,akitoa salamu za Mkoa wake wakati wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unaofanyika leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano wa Wadau kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini zinazotekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu zinazotekeza mradi huo katika maeneo yao.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 28,2023 jijini Dodoma na Mhe.Majaliwa katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Wadau Kujadili Utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.
‘’Ili mradi ufanikiwe ni vyema wadau wakashiriki kikamilifu katika mradi na nieendelee kuhimiza wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kutoa ushirikiano kwa timu za utekelezaji mradi’’ amesema Mhe. Majaliwa
Hata hivyo Mhe.Majaliwa amezitaka Taasisi zinazofanya kazi na mradi kama vile NIDA, NEMC, Tume ya Matumizi ya Mipango Bora ya Ardhi na taasisi zote kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi.
Amesema kuwa Januari 21, 2022 serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilisaini makubaliano na Benki ya Dunia ya mkopo wa Sh.bilioni 346 sawa na dola za kimarekani milioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
“Mradi huu unatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano na una vipengele vinne ambavyo ni kuongeza usalama wa milki,kuimarisha mifumo ya taarifa za ardhi, kujenga miundombinu ya ardhi na usimamizi wa mradi”amesema
Aidha Mhe.Majaliwa, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri katika kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha, watenge bajeti kupunguza migogoro ya ardhi.
“Nawaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini katika kipindi hiki cha maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2024/25 watenge fedha kwa ajili ya sekta ya ardhi ili kuendeleza utekelezaji wa mradi katika maeneo yale ambayo mradi haujaweza kufika.
Ameongeza “Watalaam wa sekta ya ardhi washirikiane na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kuwapa wananchi elimu kuhusu masuala ya ardhi ili kupunguza migogoro iliyopo.”amesema
Kwa upande wake Waziri wa Madini ambaye ni mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa mradi huo utasaidia kuondoa changamoto za ardhi pamoja na kuwahakikishia wananchi umiliki wa maeneo yao kwa matumizi mbalimbali.
”Mradi huo umekuja wakati muafaka na kubadilisha maisha ya mtanzania.”amesema Mhe.Mavunde
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi.Rosemary Senyamule amesema kuwa kutokana na serikali kuhamashia makao makuu Dodoma uhitaji wa ardhi umekuwa mkubwa.
“Tunampomgeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu ambao utasaidia kuongeza usalama wa milki za ardhi na kutatua migogoro iliyopo katika maeneo mbalimbali,” amesema Bi.Rosemary
Awali Kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga amesema hadi kufikia Novemba 20 mwaka huu, viwanja 21,889 vilikuwa vimetambuliwa.
Mhandisi Sanga amefafanua kuwa kati ya hivyo, viwanja 11,068 upimaji wake umekamilika na vipo katika hatua ya maonyesho kwa umma ili kutoa fursa kwa wananchi kuhakiki na kurekebisha taarifa zao.
Aidha amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha wizara kupitia mradi huo imelenga kukamilisha urasimishaji wa makazi 500,000 ambapo kati ya hayo makazi 100,000 yatarasimishwa kwa kutumia watumishi wa umma na makazi 400,000 kupitia makampuni binafsi ya upangaji na upimaji .
“Zabuni za upatikanaji wa makampuni yatakayofanya kazi ya urasimishaji zipo hatua za mwisho,”amesema Mhandisi Sanga