Mwenyekiti wa ITY Kanda ya ziwa Oliva Gaitani (kulia) akigawa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwanza na Pamba zilizoko Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza.
Katibu wa Mbunge Jimbo la Ilemela Mkoani mwanza Charles David akiwa ameshika Keki na wanachama wa ITY Mwanza B ikiwa ni ishara ya uzinduzi.
Kiongozi wa ITY Kanda ya ziwa Frida Betty akigawa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mihama iliyoko Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza.
Katibu wa Mbunge Jimbo la Ilemela Mkoani mwanza Charles David akigawa vyeti kwa washiriki waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa ITY Mkoa wa Mwanza na Geita
Katibu wa Mbunge Jimbo la Ilemela Mkoani Mwanza Charles David akizungumza kwa niaba ya Mbunge Dkt.Angelina Mabula kwenye hafla ya uzinduzi wa ITY Mkoa Mwanza na Geita
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kikundi cha Itambue Thamani Yako (ITY) kimetoa taulo za kike kwa shule za Sekondari Mkoani hapa za Mwanza,Pamba,Mihama na Ibungilo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau wengine za kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa na hedhi salama.
Wakizungumza mara baada ya zoezi la ugawaji wa taulo za kike lililofanyika shule ya Sekondari Mwanza baadhi ya wanafunzi wanaeleza namna ambavyo taulo hizo zitawasaidia kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wakati wa hedhi.
Gloria Masunga ameeleza kuwa wanapokosa taulo za kike kwaajili ya kujistiri wanashindwa kujiamini hali inayopelekea kushindwa kufika shuleni.
Ameeleza kuwa ITY wamefanya kitu kizuri na kwa msaada walioutoa umewafanya wajione wa thamani na watajiamini wakati wote wanapokuwa shuleni.
Edith NGoroma ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Pamba, ametoa rai kwa wazazi kuhakikisha wanatenga bajeti kwaajili ya taulo za kike kwa watoto wao waweze kujistri ili waepukane na utoro.
“Watoto wanapochafua nguo wakiwa kwenye hedhi huwa wanashindwa kujiamini na wanaogopa hata kukaa darasani, hivyo wazazi mjitahidi sana kutenga fedha kwaajili ya kuwanunulia taulo za kike ili waweze kuhudhuria masomo yao bila kikwazo chochote”, amesema Mwalimu Ngoroma
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ITY Kanda ya ziwa Oliva Gaitani, amesema kikundi chao kipo nchi nzima na lengo kubwa ni kuwafundisha wanawake kujipenda, kujiamini na kushiriki katika shughuli za kijamii sanjari na kutoa tabasamu kwa watu wasiojiweza kama walivyogawa taulo za kike kwa wanafunzi.
“Leo tupo hapa Mwanza kwaajili ya ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi pamoja na uzinduzi wa tawi jipya la ITY Mwanza B na Geita”, amesema Gaitani
Amesema uhitaji wa taulo za kike ni mkubwa hususani kwa watoto waliopo mashuleni, kutokana na uhitaji huo ameiomba Serikali iweke utaratibu wa kutoa taulo hizo bule ili watoto waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Naye kiongozi wa ITY Kanda Frida Betty amesema pamoja na kutoa taulo za kike pia wanatoa elimu ya matumizi ya taulo hizo ili watoto wazingatie suala zima la usafi.
“Sisi kama ITY tunaamini mtoto wa kike akiwezeshwa anaweza,niwaombe wadau wengine mjitoe kwaajili ya kuwasaidia watoto wetu ili waweze kutimiza ndoto zao”, amesema Betty
Awali akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angelina Mabula mara baada ya kuzindua ITY Mwanza ‘B’ na Geita Katibu wa Mbunge Charles David, amewapongeza wanachama wa ITY kwanamna ambavyo wanatoa tabasamu kwa watu wasiojiweza.
David amesema kwakutambua shughuli wanazozifanya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angelina Mabula atawasaidia vifaa vya Steshenali ikiwemo Kompyuta ili viweze kuwasaidia kurahisisha shughuli zao kwa wakati.
“Wanawake ni Jeshi kubwa na mkiamua jambo lenu iwe mvua au jua lazima mlikamilishe hivyo nawapongeza sana kwa hatua hii mliofikia na Mheshimiwa Mbunge yuko tayari kushirikiana na nyie wakati wowote mnapokuwa na jambo lenu msisite kumshirikisha”, amesema David