……..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa uongozi wa mkoa wa Songwe uhakikishe unakamilisha miradi yote ambayo ilikwishapatiwa fedha kutoka Serikali Kuu lakini bado haijakamilika hadi sasa.
“Leo ni Novemba, natoa miezi mitatu ikifika Februari 28, mwakani miradi yote ambayo fedha zilikuja tangu mwaka 2021 na haijakamilishwa iwe imekamilika. Vinginevyo, nachukua hatua kali,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Novemba 25, 2023) wakati akizungumza na viongozi wote wa mkoa huo kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake mkoani humo.
Amesema Wakurugenzi Watendaji wote waliopo ni wageni lakini wa zamani ni lazima watafute ili waje kujibu hoja. “Miradi hii haikuja hapa tu, iko nchi nzima. Kuna maeneo hata zahanati hazijaisha, kwani inahitaji mabati mangapi? Ni kwa nini haijakamilika?” amehoji.
Waziri Mkuu ambaye amemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu, amemkabidhi Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Francis Michael orodha ya miradi yote ambayo bado haijakamilishwa ili aisimamie.
Akitoa mifano ya miradi hiyo wilayani Mbozi, Waziri Mkuu amesema kuna bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Lutumbi ambalo sh. milioni 80 zilitolewa tangu mwaka 2021/2022 lakini hadi leo halijaisha.
“Shilingi milioni 350 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kufulia, la upasuaji na wodi ya mama na mtoto katika kituo cha afya Itaka bado havijakamilika. Kituo cha afya Arya Nambizo kilipewa shilingi milioni 500 hakijaisha, kituo cha afya Hezya kilipata shilingi milioni 500 haijaisha na zahanati ya Chizumbi ilipata sh. milioni 50, nayo haijaisha.”
Amesema wilayani Momba kuna shule ya sekondari Ikala ambayo ilipelekewa sh. milioni 470 lakini maabara bado hazijakamilika. “Kuna kituo cha afya Msagala, kilipata sh milioni 500 lakini bado milango haijawekwa. Pia sh. milioni 500 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto kwenye hospitali ya wilaya hiyo lakini halijaisha. “
Wilayani Ileje, Waziri Mkuu amesema shilingi milioni 500 zilitolewa kwa ajili ya kituo cha afya Ndola lakini nacho hakijaisha. Kwenye kituo cha afya Itala, zililetwa sh. milioni 500 kwa ajili ya wodi tatu lakini hadi leo ya wanaume haijaanza. Na kwenye shule ya sekondari Ibanda, tangu mwaka 2021 walipata fedha za kujenga madarasa mawili ya maabara lakini nayo hayajakamilika,” amesema.
“Wilayani Songwe nako iko miradi ambayo haijakamilika. Ni nini kimekwamisha haya majengo yasiishe? Fedha imekuja kama ambavyo ilienda kwenye maeneo mengine, na fedha hizi zimeenda hadi Katavi lakini wamekamilisha. Mbozi na Katavi wapi kuna mazingira magumu ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi?” alihoji na kuongeza kwamba tatizo kubwa ni udhaifu uliopo kwenye idara za manunuzi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Wilaya wapite kwenye shule za bweni na kuangalia kama michango holela bado inaendelea kutozwa.
“Kuna shule hapa Mbozi jana niliwasomea watumishi ambayo inatoza michango ya hovyo dhidi ya nia njema ya kuchangia chakula. Kwa utaratibu uliopo, hii michango ni lazima ijulikane kwa Afisa elimu wa wilaya, Mkurugenzi na ithibitishwe na Mkuu wa Wilaya husika,” amesisitiza.
Jana katika kikao hicho, Waziri Mkuu aliwasomea fomu ya kujiunga na sekondari ya Nalyele ambapo wazazi wanatakiwa kuchangia fedha ya chakula kila mwezi lakini yameongezeka mahitaji mengine ikiwemo fedha za ukarabati, ulinzi, kulipa wapishi, bili za maji na umeme, posho ya walimu 15,000/-, posho ya matron/patron, vifaa vya usafi, posho ya kamati ya wazazi ambavyo jumla yake ilikuwa ni zaidi ya sh. 350,000/-.
“Nimeiita ni michango ya hovyo, kwa sababu Mkuu wa Shule anatoza michango kisha anawalipa posho walimu, patron au matron. Pia wameingia bili za maji na umeme, ulinzi na ukarabati wa majengo wakati fedha hizo ziko kwenye ruzuku ya uendeshaji (Capitation Grant) ambayo kila mwezi inatolewa na Serikali.”