Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) lililopo nchini Australia wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kupandikiza valvu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku sita iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wagonjwa 25 watoto 16 na watu wazima tisa walifanyiwa upasuaji katika kambi hiyo.
Mtaalamu wa kuendesha mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung Machine) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Lujani Hoho akiendesha mashine hiyo wakati wa kambi maalumu ya siku sita inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia.
Picha na: JKCI
Na: Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Magonjwa ya kinywa, meno na njia ya hewa kama hayatatibika kikamilifu yanaweza kusababisha matatizo ya watu kupata magonjwa ya valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo.
Kambi hiyo ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima imefanywa na wataalamu wa moyo wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia.
Dkt. Angela alisema magonjwa ya valvu za moyo yamekuwa tatizo kubwa hapa nchini kutokana na idadi ya wagonjwa hao kuongezeka kutokana magonjwa ya mafua na kifua kutotibiwa vizuri.
“Mgonjwa mwenye matatizo ya valvu za moyo hupata tatizo hilo akiwa na umri mdogo na baadaye kuanza kuonyesha dalili za kupata madhara kwenye moyo hivyo kupelekea valvu kuvujisha damu au valvu kufunga na kutokupitisha damu vizuri”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi alisema matibabu ya matatizo ya valvu hufanyika kwa kubadilisha na kuweka valvu za bandia ili kuiruhusu damu kuzunguka kwenye moyo kama inavyotakiwa.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo ambapo wagonjwa 25 watoto wakiwa 16 na watu wazima tisa walifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo Dkt. Angela alisema wataalamu wa JKCI pia walipata mafunzo ya jinsi ya kufanya upasuaji wa moyo kwa watu wazima wenye matatizo ya valvu za moyo.
“Upande wa matibabu ya watoto, katika kambi hii tumetoa huduma kwa watoto wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, kurekebisha mishipa ya damu pamoja na kuwafanyia upasuaji wa mara ya pili watoto ambao tayari walishafanyiwa upasuaji”, alisema Dkt. Angela.
Naye daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia Dkt. Hugh Wolfenden alisema wanashirikiana na JKCI kuongeza ujuzi kwa wataalamu wanaotoa huduma za upasuaji wa moyo pamoja na kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma za upasuaji wa moyo.
Akizungumzia kuhusu matatizo ya valvu za moyo Dkt. Wolfenden alisema nchini Austaria wangonjwa wenye matatizo ya valvu za moyo wamepungua kutokana na elimu inayowekezwa katika jamii tangu utoto kuhusu afya ya kinywa na meno.
“Nchini Australia elimu kuhusu afya ya kinywa na meno inatolewa mara kwa mara ili kuhakikisha jamii inakuwa na mazoea ya kupiga mswaki kila baada ya kula chakula, umuhimu wa kukaa maeneo masafi na yasiyo na msongamano ili kuzuia magonjwa ya mfumo wa hewa yanayoweza kupelekea kupata magonjwa ya valvu za moyo”,.
“Nimeshafanya kazi kwa kipindi cha miaka 32 sasa, idadi ya wagonjwa wenye matatizo ya valvu za moyo Australia ni wachache kwa sasa kwani jamii inajikinga zaidi kuepuka kupata magonjwa yanayosababishwa na afya ya kinywa” na meno, alisema Dkt. Wolfenden