Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba, akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Singida yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (TAMISEMI) yaliyoanza leo Novemba 23, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WATENDAJI wa Kata na Maafisa Tarafa
wa Mkoa wa Singida wametakiwa kufanya kazi kama timu ili kuondoa misuguano
isiyo ya lazima wakati wa utendaji wa kazi za kuwahudumia wananchi kwenye
maeneo yao.
Ombi hilo limetolewa na Mhadhiri kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo ki;ichopo Dodoma, Paul Faty wakati akitoa mada kwenye mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea
uwezo maafisa hao yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mtaa (TAMISEMI) yaliyoanza leo Novemba 23, 2023.
Faty alisema mara nyingi kumekuwa kukitokea muingiliano katika utendaji wa
kazi kwa maafisa hao na kusababisha kushindwa kufanya kazi ipasavyo za
kuwahudumia wananchi kutokana na sababu mbalimbali.
“Kufanya kazi kama timu na kushirikishana kutawafanya muweze kuwahudumia
wananchi vizuri katika maeneo yenu kwa kusimamia utekelezaji wa sera, sheria
kanuni na miongozo ya Serikali ,” alisema Faty.
Aidha, Fati alisema kuwa moja ya majukumu wanayopaswa kuyafanya ni kuwasikiliza
wananchi na kutatua kero zao kwani wao ndio waliopewa dhamana ya kuonana nao moja
ka moja na ni kiunganishi kati yao na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ambaye alimwakilisha
Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba kufungua mafunzo hayo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi na
maarifa wakati wa kutekeleza majukumu
yao ili kupunguza kama siyo kuziondoa kabisa changamoto wanapo wahudumia wananchi
na kuimarisha mahusiano baina yao na Serikali.
Mragili aliwakumbusha baadhi ya majukumu yao maafisa Tarafa na watendaji hao
wa kata kuwa ni pamoja na kumwakilisha na kumsaidia mkuu wa wilaya katika
utekelezaji wa shughuli za Serikali kuu na Taifa, kuhamasisha wananchi
kushiriki shughuli za maendeleo kwenye Tarafa zao na kuwa kiungo cha wananchi
na kata husika.
Mambo mengine aliyowakumbusha ni kushughulikia malalamiko ya wananchi
katika Tarafa, kufuatilia na kuhimiza utekelezaji wa Sera za Serikali katika
maeneo yao na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo, kushiriki katika kupanga
miradi ya maendeleo katika kata na kuwa mtendaji mkuu wa kata ni kiungo wa
idara zote katika kata.
Alitaja mambo mengine aliyowakumbusha maafisa hao kuwa ni kuandaa mpango
kazi wa maendeleo katika kata na kuhuwasilisha kwa mkurugenzi na Afisa Tarafa,
kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria kanuni na miongozo ya
Serikali katika kata, mratibu wa upangaji wa mipango shirikishi ya maendeleo
katika kata na kupokea na kutatua malalamiko na matatizo ya wananchi katika
kata.
Naye Naibu Mkuu wa chuo hicho Dkt. Michael Msendekwa akizungumza kwa niaba
ya mkuu wa chuo hicho, alisema chuo hicho kilianzishwa kwa sheria namba 26 sura
396 lengo kubwa likiwa ni kuziwezesha mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze
kutekeleza majukumu yake.
Alisema chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu yenye
programu sita kuanzia ngazi ya cheti na sasa wanatoa shahada ya kwanza na kueleza
kuwa kimejipanga kuiwezesha Serikali za Mitaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya TAMISEMI, Hamisi Mkanga
alisema mafunzo hayo yalianzishwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo maafisa Tarafa
na watendaji kuanzia ngazi ya chini kabisa ndipo walipo omba chuo hicho
kiwatafutie mada ambazo zitaendana na maafisa hao kwa kukumbushana mambo
mbalimbali.
Alisema mafunzo hayo ya siku mbili yatawashirikisha walengwa hao katika
mada mbalimbali ambazo wataweza kuzifanyia kazi.
Alisema mada ambazo watafundishwa ni takribani 13 na kuwa mafunzo hayo kwa
awamu ya kwanza yalifanyika mikoa ya Katavi, Rukwa, Njombe pamoja na Songwe na
kwa awamu hii ya pili kuna mikoa ya Singida, Shinyanga, Tabora, Pwani, Dar es
Salaam, Lindi pamoja na Mtwara na kuwa wataendelea kutoa mafunzo hayo kwenye
mikoa mingine kulingana na jinsi watakavyokuwa wanapata fedha.
Mkanga alitumia nafasi hiyo kuwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia
mada wanazofundishwa kwani ni za muhimu sana.
Baadhi ya mada zilizofundishwa kwa siku ya kwanza ni Uongozi na Utawala,
Sera na Sheria zinazosimamia Tawala za Mikoa na MSM, Maadili ya Utumishi wa
Umma, Majukumu ya Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa, Muundo, mfumo wa
uwajibikaji na mawasiliano Serikalini na mafunzo ya awali ya MUKI.
Mada zitakazo fundishwa siku ya pili ni Upangaji mipango na
Bajeti, Usimamizi na Udhibiti wa Fedha, Usimamizi na Ununuzi wa Umma,,
Usimamizi wa Miradi, Ushughulikiaji Malalamiko (kero za wananchi), Kuhabarisha
Wananchi Mafanikio ya Serikali, Mfumo wa Kujifunza Kielektroniki (MUKI) na
Utunzaji wa Siri za Serikali.
Naibu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Dkt. Michael Msendekwa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa chuo hicho wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.