Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akizungumza na wananchi wa kata ya Upolo Wilayani Nyasa alipoenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo inajengwa na Serikali kupitia kupitia mradi wa SEQUIP.
Na: James Mwanamyoto-Nyasa
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amempongeza mkazi wa Kata ya Upolo Wilayani Nyasa Bw. Adakick Alex Milinga kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa eneo ambalo Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo inajengwa ili kutatua changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Dkt. Msonde ametoa pongezi hizo kwa mwananchi huyo, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Upolo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya sekondari inayojengwa na Serikali kupitia mradi wa SEQUIP katika kata hiyo Upolo Wilayani Nyasa.
Dkt. Msonde amesema taifa likipata wananchi wanaojitoa katika kumuunga mkono kwa vitendo Mhe. Rais kama alivyofanya Bw. Adakick Alex Milinga ni wazi kuwa taifa litapiga hatua ya maendeleo kwa kasi kubwa.
“Kitendo cha Bw. Milinga kutoa eneo lake tena kwa hiyari yake ili shule ijengwe maana yake ni kwamba anaunga mkono kwa vitendo jitihada za Mhe. Rais kuboresha miundombinu ya elimu ili watoto wa kitanzania wapate elimu bora,” Dkt. Msonde amefafanua.
Dkt. Msonde amesisitiza kuwa, mchango alioutoa Bw. Milinga hautasaulika kamwe kwani hata maandiko matakatifu yanasema mtu anayetoa kitu kuisaidia jamii inayomzunguka atapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Aidha, Dkt. Msonde amempongeza Mhandisi Allen Mshiu kwa kusimamia vema ujenzi wa shule hiyo mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo ambayo ujenzi wake unaendelea vizuri kwa kuzingatia viwango na thamani halisi ya fedha iliyotolewa.
“Nimeona namna Mhandisi Allen Mshiu alivyosimamia ujenzi vizuri, majengo yamewekewa msingi imara pamoja na nguzo imara hivyo naamini yatadumu kwa muda mrefu,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Ili ujenzi ukamilike kwa wakati, Dkt. Msonde ameelekeza mafundi wa kutosha waongezwe, kazi za ujenzi ambazo hazitegemei kukamilika kwa nyingine ndio zianze kufanywa ziendelee kutekelezwa ikiwa ni pamoja na ujenzi kufanyika usiku na mchana ili kwenda na muda.
Katika kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo yake, Dkt. Msonde amewaahidi wananchi wa Kata ya Upolo kuwa, atarejea tarehe 10, Disemba, 2023 kwa ajili ya kukabidhiwa rasmi shule hiyo ili ianze kutumika kama Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyokusudia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mhe. Filberto Sanga amesema kuwa, pindi Dkt. Msonde akirejea tarehe 10, Disemba 2023 atamuomba amkabidhi hati maalumu Bw. Adakick Alex Milinga ya kutambua mchango wake wa kutoa eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo, ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa wananchi wengine kujitoa katika kuchangia maendeleo.
Mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo ulianza tarehe 28 Agosti, 2023 ambao utagharimu kiasi cha shilingi 560,552,827/= ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi 281,778,505/= kimeshatumika katika ujenzi na kiasi cha shilingi 278,774,322/= kimesalia kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akizungumza na wananchi wa kata ya Upolo Wilayani Nyasa alipoenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo inajengwa na Serikali kupitia kupitia mradi wa SEQUIP.
Wananchi wa kata ya Upolo Wilayani Nyasa wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) alipozungumza nao mara baada kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo inajengwa na Serikali kupitia kupitia mradi wa SEQUIP.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akimpongeza mkazi wa Kata ya Upolo Wilayani Nyasa Bw. Adakick Alex Milinga kwa kutoa eneo ambalo Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo inajengwa na Serikali kupitia kupitia mradi wa SEQUIP.
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akielekea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Upolo inajengwa na Serikali kupitia kupitia mradi wa SEQUIP.