Na Aron Msigwa – WUSM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kulinda na kutunza maeneo yenye historia ya wapigania Uhuru waliotoa maisha na mali zao kwa ajili ya Ukombozi wa Bara la Afrika na kukiagiza Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kilichopo jijini Dar es salaam kiandae mpango wa kuyakarabati makaburi ya Kinondoni walipozikwa baadhi ya wapigania uhuru.
Ameyasema hayo leo Novemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam alipotembelea makaburi hayo kwa lengo la kupata historia ya mchango wa wapigania uhuru na kuona namna Wizara kupitia Kituo hicho itashirikiana na Manispaa ya Kinondoni kuhifadhi historia hiyo.
“Hapa ni mahali panapoonesha kuwa, Tanzania ilishiriki katika Ukombozi wa Bara la Afrika, wapo Watanzania wengi walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika Ukombozi wa Bara la Afrika ambao pia walizikwa katika maeneo mengine hapa nchini. Naomba muendelee kulitunza eneo hili, hiki ni kelelezo muhimu ambacho kitaishi milele. Nakiagiza Kituo cha Urithi wa Ukombozi kitafute fedha ili kuliboresha eneo hili ili liendelee kuwa kumbukumbu muhimu kwa nchi yetu”
Aidha, Katibu Mkuu Msigwa amekiagiza Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kifanye Utafiti nchi nzima ili kubaini maeneo ya historia walipozikwa wapigania uhuru pia kiyafuatilie maeneo mengine hapa nchini ambayo yana historia ya wapigania uhuru.
“ Baadhi ya maeneo yamekuwa mashamba ya watu, kuna watanzania wengi ambao wametoa mchango mkubwa katika Ukombozi wa nchi nyingine, tuna wajibu wa kuyatafuta, kuyahifadhi na kuyatunza ili jamii iyajue na kuendelea kuenzi na kujifunza harakati na uzalendo walizozifanya wapigania uhuru hao” amesisitiza Bw. Msigwa.
Ameeleza kuwa, katika kipindi cha sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza harakati hizo ambazo sasa zimehamia katika harakati za Ukombozi wa wananchi kiuchumi.
Amesema Wizara hiyo, iko tayari kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni na taasisi nyingine ambazo zina maeneo ya wapigania uhuru ili kuyahifadhi ili yaendelee kuwa historia, eneo la mafunzo na ibada kwa Watanzania pia kivutio cha Utalii wa historia akitoa wito kwa wadau mbalimbali walete Mawazo ya namna bora ya kuliboresha Zaidi eneo hilo ili liendelee kuwa chimbuko la historia.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Kinondoni Bw. Songoro Mnyonge amesema eneo hilo lilikabidhiwa katika Manispaa hiyo mwaka 2000 likiwa na makaburi 23 ambapo 21 ni ya wapigania Uhuru wa ANC na PAC na 2 ni ya wapigania Uhuru wa nchi ya Msumbiji akiwemo mke wa kwanza wa Rais wa Msumbiji Mama Josina Abiathar Muthemba Machel.