Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 22, 2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu utaratibu na hatua za uhimizaji ulipaji wa kodi za pango.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeingia makubaliano na Dalali wa Mahakama kwa ajili ya kukusanya madeni shilingi bilioni 7.8 kutoka kwa wapangaji wao ambapo kwa mujibu wa sheria fedha hizo zinaitajika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
Kampuni hiyo ya udalali wa Mahakama ni WINS Auction Mart ambayo imeshakabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa kuanzia Desemba Mosi mwaka huu.
Huku hatua itakayofuata mara baada kuondolewa katika nyumba hizo kuwafungulia kesi za madai mahakamani wadaiwa hao ili kuhakikisha wanalipa madeni hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 22, 2023 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro, amesema kuwa
hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu TBA inadai zaidi ya bilioni 7.8 za kodi ya pango kutoka kwa wapangaji wa nyumba na majengo.
Arch. Kondoro amesema kuwa nyumba na majengo hayo yanayomilikiwa na TBA, huku akieleza kuwa zaidi ya bilioni 3.5 ni madeni ya Taasisi mbalimbali za serikali.
Amesema kuwa ulimbikizwaji wa madeni hayo kumekuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya maendeleo ikiwemo kujenga nyumba mpya kwa ajili ya kupangisha au kuuzwa pamoja na kukarabati nyumba zilizopo.
Amesema kuwa hatua ya kuwaondoa wadaiwa sugu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambaye amepewa zabuni hiyo kwa niaba ya TBA zitaendelea.
“Madeni haya ni ya mwaka wa Fedha uliopita, mikoa kinara ni taasisi za Umma katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya ambayo deni limefikia shilingi Bilioni 1.4” amesema Arch. Kondoro.
Arch. Kondoro ameeleza kuwa; Kuanzia Desemba 1, 2023, TBA itaanza kutumia mfumo mpya wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) toleo la 2.
“Mfumo huu mpya utakuwa unatoza riba ya 20% kwa mpangaji atakae kaa zaidi ya miezi 3 bila kulipa kodi ya pango. Riba hiyo itaendelea kutozwa kila mwezi kwa kiwango mfuato (automatically) cha 20% mpaka deni lote litakapokamilika kulipwa.”Arch. Kondoro