Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa
tiba Mkoa wa Singida vyenye jumla ya takribani Sh.Milioni 222.472.
Vifaa hivyo ni pamoja na majenereta, sambamba na vifaa vitakavyotumika
kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya muda na huduma nyinginezo ambavyo vimekabidhiwa
kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kituo cha Afya Sepuka na Hospitali ya
Wilaya ya Singida, Ilongero.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambayo ilishuhudiwa na
wabunge, watendaji wa idara mbalimbali za sekta ya afya, wananchi pamoja na
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Meneja
wa MSD Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa alisema kazi hiyo ya usambazaji
wa vifaa hivyo ni jukumu lao walilopewa na Serikali.
” Kazi yetu kubwa sisi MSD ni Kununua, Kuzalisha, Kuhifadhi na Kusambaza bidhaa za Afya na vitendanishi
hapa nchini ambayo tunaifanya kwa mamlaka ya kisheria,” alisema Jumaa.
“MSD leo tupo hapa Ikungi kwa ajili ya kukabidhi jenereta, kitanda cha kufanyia upasuaji, Ultra-Sound mashine pamoja na mashine
ya kuasaidia kuwapatia joto watoto wachanga na waliozaliwa kabla ya wakati.(njiti) (Infant Rad warmaer) vyenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 72
Jumaa alisema lengo kubwa la kupelekwa kwa vifaa
hivyo ni kuhakikisha huduma za uzazi zinaboreshwa na kuwa katika wilaya hiyo
MSD ilikuwa inakamilisha vifaa ambavyo ilikuwa imepokea fedha zaidi ya Sh.
Milioni 300 ili kukamilisha usambaji wake.
Alisema MSD Kanda ya Dodoma imepokea maombi ya vifaa tiba vyenye zaidi ya walipokea zaidi ya Sh. Milioni
700 ambapo pia kuna vifaa vya zaidi ya 700 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ajili ya vituo vya Afya na Zahanati.
“Ukiangalia muda tuliopokea fedha hizi na
utekelezaji wa kupeleka vifaa hivyo ni muda mfupi sana na hiyo imetokana na
Serikali kuboresha huduma za MSD na kufikia hatua hii ya kukamilisha vifaa
ambavyo hatukuvipeleka awali na kuvipeleka sasa baada ya fedha zake kuzipokea muda
mfupi uliopita,” alisema Jumaa.
Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha na MSD imekuwa
ikinunua na kusambaza vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kote nchini
ambapo aliishukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa inajenga morali kwa watumishi
wa sekta ya afya na kuipenda kazi wanayoifanya.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji
Mtaturu aliishuru Serikali na MSD kwa
kupeleka vifaa hivyo na kueleza kuwa sekta ya afya ni uhai na kuwa watu wakiwa
na afya njema ndipo wataweza kufanya kazi zao vizuri.
“Leo hii tunashuhudia vifaa hivi vilivyo letwa
na Serikali kupitia MSD na kukabidhi hospitali yetu ya Ikungi maana yake ni
utekelezaji wetu wa kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo tuliiomba kwa muda
mrefu,” alisema Mtaturu.
Alisema kujenga majengo tu ya hospitali haitoshi na
kuwa inahitaji na vitu vya ziada vikiwemo vifaa na kuwa madaktari na wataalamu
wengine wamesomeshwa kwa lengo la kuwasaidia watu kutibu maradhi mbalimbali na kwa
kuvitumia vifaa hivyo ndio wanaweza kufanya kazi yao kwa urahisi iwe kwa kupima
na kufanya upasuaji.
Mtaturu alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya afya hapa nchini
hivyo kila mtu mpenda maendeleo anapaswa kumshukuru kwa jinsi anavyo iendesha
nchi kwenye sekta mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki
Kingu akipokea vifaa hivyo kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Sepuka alisema miongoni mwa vifaa alivyo
pokea kutoka MSD ni jenereta lenye ukubwa wa KVA 60 na vifaa vingine 11 ambavyo
baadhi ni toroli la kuwekea vifaa wakati madaktari na wauguzi wanapokwenda
kutoa huduma, vifaa vinavyotumika kumsaidia mtoto baada ya kuzaliwa aweze
kupumua vizuri na kuwa vifaa vyote alivyovipokea vinatumika kupingana na uzazi
pingamizi na lengo lake ni kumuokoa mama wala mtoto wasife wakati wa
kujifungua.
Alitaja vifaa vingine alivyopokea ni mashine kwa
ajili ya hewa, mashine ya kupimia uzito, kifaa cha kutundikia dripu ya maji,
kifaa cha kuwapa joto watoto waliozaliwa kabla ya muda, kifaa cha kuvuta uchafu
kwenye njia ya hewa baada ya mtoto kuzaliwa, saa ya ukutani, kifaa kinachobeba
vifaa vya kumuhudumia mtu aliyepata majeraha na pampu inayotumika kumnyonya
mtoto kwa ajili ya kuondoa kitu kilichokwama kooni au kupoteza fahamu baada ya
kupaliwa na kuwa vifaa hivyo vyote vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 82.
Kingu aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha na
akapongeza maboresho makubwa yaliyofanywa ndani ya MSD na kueleza kuwa MSD ya
leo ni ya kisasa na mkombozi kwa wananchi katika kazi ya kutoa huduma za afya
si kwa Mkoa wa Singida pekee bali kwa nchi nzima kazi ambazo zimekuwa
zikionekana kupitia vyombo vya habari.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Singida
Kaskazini, Ramadhani Ighondo aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea jenereta na
gari la kuwabebea wagonjwa na wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza
maisha kutokana na kukosa umeme wa uhakika wakati wakipata huduma hasa za
upasuaji na kukosekana kwa gari la kuwapeleka hosptali wanapokuwa wagonjwa.
Ighondo alisema pamoja na kupelekewa gari hilo pia
Serikali kupitia MSD imewapelekea kifaa kinachotumika kwa ajili ya kuwaongezea
joto watoto wanaozaliwa chini ya muda.
Alisema mbali ya gari hilo la wagonjwa vifaa
walivyopokea vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 62.7
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dorisila Mlenga,
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu pamoja na Mganga Mfawidhi
wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel waliishukuru Serikali kwa kuwapelekea
vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kuwarahisishia utendaji wa kazi za kutoa huduma
kwa wananchi ambapo walisema watavisimamia na kuvitunza ili viweze kudumu kwa
muda mrefu wakizingatia Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.
Wananchi Elesisia Mlenga, Asha Salim, Asha Musa,
Mwalimu Tatu Njoka, Ashura Iddi na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Seketoure, Getruda Yona waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapekea jenereta na gari la wagonjwa na kueleza kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuwasaidia
katika kupata huduma bora za afya.
Mwanafunzi Getruda Yona alimshukuru Rais Samia kwa
kuwajengea shule na kuwapunguzia umbali mrefu ambapo walikuwa wakitembea zaidi
ya kilomita 10 kwenda shuleni kabla ya kujengewa kwa shule hiyo ya Seketoure.
Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu ikiwa ni ishara ya kumkabidhi genereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD katika hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Kituo cha Afya cha Sepuka Wilaya ya Ikungi. Kutoka kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel , Diwani wa Kata ya Sepuka Halima Ng’imba, Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja MSD Kanda ya Kati, Juliana Mbogo na Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.
Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akisisitiza jambo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Mbunge wa Jimbo la Singida, Magharibi Elibariki Kingu (kushoto) Kulia ni Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa MSD Kanda ya Kati, Juliana Mbogo.
Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akipeana mkono na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Sepuka Kesia Daniel baada ya kukabidhi vifaa hivyo.
Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akiwa katika picha ya pamoja na wanawake waliohudhuria kliniki wakati wa makabidhiano ya vifaa hvyo Kata ya Sepuka.