Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyowapatia fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ole Sendeka ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye ziara ya siku moja ya Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde, alipotembelea mji mdogo wa Mirerani.
Amesema katika kipindi kifupi cha utawala wa Rais Dkt Samia, miradi mingi imetekelezwa wilayani Simanjiro, hivyo hawana kitu cha kumlipa zaidi ya asante na kumpa kura nyingi za ndiyo mwaka 2025.
“Rais Dk Samia ametufanikisha kwa fedha zake miradi ya maji, zahanati mpya 11 hapa Simanjiro, miradi ya barabara ya lami ikiwemo ya kutoka Arusha inayopita Simanjiro, Kiteto hadi Kongwa mkoani Dodoma,” amesema Ole Sendeka.
Amesema hata barabara ya lami ya kilomita moja, kutoka mji mdogo wa Mirerani, hadi lango la kuingia kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite, imeanza kujengwa ambayo imekaguliwa na Waziri Mavunde.
“Pamoja na hayo tunampongeza Waziri Mavunde ambaye amekuja na kauli mbiu yake ya Vision 2030 madini ni maisha na utajiri, hivyo tumpe ushirikiano wa kutosha kwenye sekta ya madini,” amesema Ole Sendeka.
Kwa upande wake, Waziri Mavunde amempongeza Ole Sendeka, kwa namna anavyofanya kazi yake ya kuwasemea wananchi wa jimbo la Simanjiro, akiwa Bungeni.
Waziri Mavunde amewasihi wakazi wa Simanjiro kumpa ushirikiano mbunge huyo Ole Sendeka, kwani ni mzoefu na mwenye upendo wa kuwatetea wananchi wake.