Na Mwandishi wetu, Mirerani
MCHIMBAJI wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Patrick Miroshi (Kipaa) amelalamika kwa Waziri wa Madini Anthony Peter Mavunde kunyanganywa mgodi wake aliouchimba kwa zaidi ya miaka 20.
Mgodi huo wa madini ya Tanzanite unaolalamikiwa na Patrick Miroshi (Kipaa) upo kwenye leseni namba PML 00416SMN ya Lema inayomilikiwa na kampuniya Njake Enterprises.
Akizungumza kwenye mkutano wa Waziri Mavunde na wadau wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani, Kipaa amesema mdhamini wake waliokuwa wakifanya naye kazi amemdhulumu mgodi wake.
“Kila mtu hapa Mirerani anafahamu kuwa mgodi ule ni haki yangu na nimekuwa masikini kwa kuuza mali zangu ikiwemo nyumba lakini mwisho wa siku nikadhulumiwa akapewa tajiri,” amesema Kipaa.
Amesema kuna mchezo mchafu ulifanyika kwa yeye kudhulumiwa mgodi wake kwa sababu hana uwezo wa kifedha hivyo Waziri Mavunde amsaidie ili aweze kupata haki yake.
“Huyu mtu ambaye nilimkaribisha alikuja akapatiwa leseni yake karibu na mgodi wangu na mwisho wa siku wakapima kwa kutumia GPS eti ikaonyesha mgodi wangu upo eneo lake,” amesema Kipaa.
Hata hivyo, Waziri Mavunde amemuagiza ofisa madini mkazi wa Mirerani (RMO) Chacha Mwita kuingilia kati suala hilo kwa kupitia nyaraka zote na kuhakikisha haki inapatikana.
“RMO fuatilia hilo kwa kuita pande zote mbili zinazohusika juu ya kuzungumzia umiliki wa mgodi huo wenye mgogoro kati ya watu hao wawili tofauti,” amesema Waziri Mavunde.
Kwa upande wake, RMO wa Mirerani Chacha ameahidi kushughulikia suala hilo kwa kuziita pande zote mbili zinazolalamikiana na kupitia nyaraka zote kisha kutoa uamuzi.
Hivi karibuni, meneja wa mmiliki wa awali wa mgodi huo Mangoshi Seleman ambaye aliuuza mgodi huo kwa Njake enterprises, Mohamed Mughanja amesema mgodi huo ni halali kwa kampuni ya Njake.
“Sisi tuliuuza mgodi huo kwa kampuni ya Njake enterprises jirani yetu akawa analalamika kuwa amedhulumiwa mgodi jambo ambalo siyo kweli na Wizara ilishatoa majibu kuwa mgodi ni wa Njake,” amesema Mughanja.