Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Mhandisi Ismail Nassor aliyenyoosha mkono,akitoa maelezo kwa baadhi ya viongozi wa jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) ya Igamba Group kuhusu ujenzi wa mradi wa maji wa Matula kijiji cha Mbozi uliotekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 230, kulia afisa maendeleo ya jamii wa Ruwasa wilaya ya Mbozi Christina Nzumba.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Mhandisi Ismail Nassor kushoto,akimsikiliza mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) ya Igamba Group Seti Nkondya kulia kuhusu faida zilizoanza kupatikana baada ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo yenye jukumu la kusimamia uendeshaji wa mradi wa maji wa Matula.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Mhandisi Ismail Nassor kulia,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Mbozi wilayani Mbozi Janeth Mwaya baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa maji Matula.
Na Muhidin Amri,
Mbozi
WIZARA ya maji kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa),imefanikisha ujenzi wa mradi wa maji wa Matula uliopo kijiji cha Mbozi Halmashauri ya wilaya Mbozi mkoani Songwe.
Mradi huo umegharimu zaidi ya Sh.milioni 230 zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uvico-19.
Kukamalika kwa mradi wa maji Matula,kumewezesha wananchi zaidi ya 2,392 wa kijiji hicho kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu na wengine kung’atwa na wadudu wenye sumu kali wakiwemo nyoka na ng’e pindi wanapokwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili.
Hayo yamesema jana na meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbozi Mhandisi Ismail Nassor,kwa waandishi wa Habari walipotembelea mradi wa maji Matula uliotekelezwa na Ruwasa kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Alisema,mradi huo umehusisha ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 75,000,kulaza bomba umbali wa kilomita 7 zilizosambazwa katika maeneo mbalimbali ya kijiji hicho,vituo 7 vya kuchotea maji na ukarabati wa chanzo kinachotumika kuzalishaji maji.
Alisema,kabla ya mradi huo wananchi wa kijiji cha Mbozi walikuwa wanachota maji kwenye chemchem na wengine kutembea umbali wa kilomita 3 kwenda kutafuta maji kwenye vijiji vya jirani.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kutoa fedha zilizofanikisha lengo la serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Mbozi Christina Nzumba alisema,mradi huo umewasaidia wananchi kupata muda wa kujikita zaidi kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii ikilinganishwa na hapo awali ambapo wananchi walitumia muda wao mwingi katika kutafuta maji.
Nzumba,amewataka wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji na miundombinu ya mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa chombo cha watumia huduma yam aji ngazi ya jamii(CBWSO) Seti Nkondya alisema,awali walitumia maji ya visima vilivyochimbwa bila kufuata ushauri wa kitaalam hali iliyosababisha wananchi kutumia maji machafu hivyo kupelekea kupata magonjwa ya kipindupindu mara kwa mara.
Alisema,sasa wananchi wana furaha kubwa kupata mradi huo na wengi wao wamehamasika kutumia maji ya bomba wanayochota kwenye vituo,kulipia huduma na wengine kuvuta maji majumbani ili kuepuka usumbufu wa kukaa muda mrefu kwenye vituo vya kuchotea maji.
Hata hivyo,ameishauri Ruwasa,kuongeza nguvu kwenye utafiti wa vyanzo vipya vya maji sambamba na uchimbaji wa visima ili kupata maji ya uhakika ili kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwenye mashamba ya kahawa.
Alisema,wilaya ya Mbozi ni maarufu kwa kilimo cha zao la hilo hapa nchini na mkombozi kiuchumi wa wananchi na serikali kwa ujumla,hata hivyo kukosekana kwa maji ya uhakika wanashindwa kulima majira yote ya mwaka na hivyo kutopata mafanikio kwenye shughuli zao za kilimo cha kahawa.