Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Ilemela Luteni Kanali Akili (wa kwanza kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala pamoja na Katibu Tawala
Luteni Kanali Akili akizungumza kwenye hafla ya wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba (Mgambo)
Hidaya Shabani mwanafunzi aliehitimu mafunzo ya Mgambo akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake
Wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba wakitembea kwa mwendo wa haraka
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Hassan Masala amewahimiza wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba (Mgambo) kuendelea kuwa rai wema kwenye jamii ili waweze kulitumikia Taifa kwa uadilifu.
Masala ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 17, 2023 wakati akifunga mafunzo hayo katika uwanja wa shule ya sekondari Lumala iliyopo Kata ya Kiseke Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza.
Amesema mafunzo waliyoyapata wakayatumie vizuri katika masuala yote ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao sanjari na kufichua uhalifu wa aina yoyote unaoendelea kwenye jamii.
Masala amesema wataendelea kuwatumia wahitimu wa mafunzo hayo katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuwapa fursa za kuwapeleka kwenye makampuni ya ulinzi ili waweze kupata ajira rasmi na zisizo rasmi.
Kwa upande wake Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Ilemela, Luteni Kanali Akili amesema mafunzo hayo yalianza Julai 3, 2023 yakiwa na wanafunzi 103 kutoka kwenye kata mbalimbali na yalifunguliwa rasmi Septemba 12, 2023 yakiwa na wanafunzi 97.
Amesema idadi ya wanafunzi iliendelea kupungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu,utoro na wengine walichaguliwa kwenda kujiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) ambapo leo wamehitimu wanafunzi 88 kati yao wanaume (76) na wanawake (12).
“Kwakipindi chote cha mafunzo wahitimu wameonesha juhudi nzuri katika nidhamu,uadilifu,uaminifu,uhodari, kupokea na kutii amri kwa wakati pamoja na uvumilivu”, amesema Luteni Akili
Akisoma risala ya wahitimu wa mafunzo hayo, Hidaya Shabani aliiomba Serikali iwapatie nafasi ya kusimamia ukusanyaji wa mapato katika Magulio,Masoko,Stendi na Bandari pamoja na kupewa nafasi za ulinzi katika shughuli mbalimbali za kiserikali zinapotokea.