Na. WAF – Arusha
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa onyo kali kwa wafamasi na wamiliki wa maduka ya dawa waotoa dawa bila kuangalia cheti cha daktari kwa kuwa kufanya hivyo ni kuendeleza tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na kuhatarisha afya za watu.
Waziri Ummy amesema hayo leo Novemba 17, 2023 wakati akifunga Kongamano la Tatu la Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa na kufungua rasmi wiki ya uhamasishaji na uelimishaji jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa inayoanza Novemba 18 hadi 24, 2023.
“Nataka wafamasia wote nchini kuacha mara moja tabia ya kutoa dawa ikiwemo za Antibiotiki bila cheti cha daktari na nikimkamata mtu siku moja nitampiga faini kubwa kama sio kumfungia duka kabisa.” Amesema Waziri Ummy.
Amesema, atatuma timu kufanya kaguzi za kushtukiza kwenye maduka ya dawa, ambapo amesisitiza mfamasia atakaebainika kutoa dawa za Antibiotiki bila cheti cha daktari atafikishwa mahakamani na atalipa faini kubwa.
Aidha, Waziri Ummy amewataka wataalamu wa Afya kuzingatia Mwongozo wa Taifa wa Matibabu wanapo wahudumia wagonjwa ili kufanikisha kampeni ya ‘Afya Moja’ yenye lengo la mapambano ya Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa.
“Naendelea kusisitiza kwa wataalam wetu wa Afya, hakikisheni mnazingatia Mwongozo wa Taifa wa Matibabu, nawaomba sana hasa katika kuwaandikia wagonjwa dawa, maana tumepata kesi tunaona mtu ana UTI anaandikiwa Antibiotic mpaka saba.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, iwapo watoa huduma za Afya watafuata Mwongozo wa Taifa wa Matibabu itawezesha Serikali kwenda kwa kasi katika mapambano ya Usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewaasa wataalam wa kilimo, uvuvi, mifugo na afya kuzingatia dhana ya mwaka huu ya Kongamano hilo kwa kuendelea kuboresha njia za mapambano ya tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa na kutoa elimu ya uwelewa kwa jamii ili kufikia lengo la mpango huo.