Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na MichezoMhe. Tabia Maulid Mwita akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na mapokezi ya Vijana wa timu ya Taifa ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 karume Boys wanaotarajiwa kuwasili Zanzibar Leo kutoka Nchini Uganda mara baada ya kukamilika kwa mechi kati ya Karume Boy na Uganda ambapo Karume BOYS walifanikiwa kuchukua ubingwa wa CECAFA U15 kwa kuwachapa wenyeji wao mikwaju ya penaalti 4 kwa 3.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepeleka ndege nchini Uganda ili kuwabeba Vijana wa Timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 15 Karume Boys kufuatia ushindi wa kombe la CECAFA.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Tabia Maulid Mwita wakati akizungumza na waandishi wa habari huko kuhusu mapokezi ya timu hiyo Ofisini kwake Migombani Zanzibar.
Amesema Rais Mwinyi amepeleka ndege hiyo ikiwa ni mwendelezo wa hamasa yake kwa timu hiyo ya Karume Boys ambayo imepambana hadi kuchukuwa ubingwa wa CECAFA baada ya kuishinda timu ya Uganda.
Waziri Tabia ameeleza kuwa Rais Dk. Mwinyi tayari ametoa shilingi milioni 5 kufuatia ahadi aliyoitoa ya kununua kila goli la Karume Boys kwa shilingi Milioni moja hivyo ametoa kiasi hicho kutokana na magoli matano yaliyofungwa na timu hiyo katika fainali hiyo.
Mbali na hayo, amesema Wizara yake pia imepokea shilingi milioni mbili kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kufuatia ahadi yake ya kununua kila goli la Karume Boys kwa Shilingi laki 5 hivyo amewaomba wadau wote walioahidi kuichangia timu hiyo wazitimize ahadi zao.
Timu ya Karume Boys imefanikiwa kushinda katika fainali hiyo kwa mikwaju ya penalt baada ya kutoshana nguvu na timu ya Uganda kwa bao 1-1.
Karume Boys inatarajiwa kupokelewa mchana huu katika viwanja vya ndege vya Karume na kutembezwa sehemu mbali mbali nchini na kuishia katika Mnara wa Kumbukumbu Kisonge.