Na. WAF – Arusha
Wataalam wa Afya ya binadamu, Afya ya mifugo na jamii wametakiwa kushirikiana ili kupambana na asilimia 70 ya magonjwa ya binaadamu yatokanayo na wanyama.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo leo Novemba 16, 2023 wakati akifungua Kongamano la Tatu la Kisayansi la Mapambano ya Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (UVIMADA) Jijini Arusha
Waziri Ulega amesema matumizi yaliyokithiri ya dawa za Antibiotiki katika kukuza mifugo kwa kuchanganya na chakula cha mifugo kwa matumizi ya kila siku kwa wanyama wanapokuwa hawaumwi hupelekea magonjwa kwa mlaji wa mfugo huo.
“Asilimia 70 ya magonjwa ya binadam yatokana na wanyama ambao nao huyatengeza kwa kupewa dawa za Antibiotiki bila utaratibu, tunapaswa kuchanja mifugo yetu kwa wakati ili iwe na kinga dhidi ya magonjwa na kuacha kuchinja mifugo inayoendelea na matibabu.” Amesema Waziri Ulega
Amesema ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anapambana na asilimia 70 ya magonjwa ya binadam yatokanayo na matumizi ya Antibiotik yaliyokithiri.
“Tatizo hili ambalo ni tishio kwa kizazi chetu kijacho sababu matokeo ya tafiti mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa za dawa nchini zinaonyesha kuwa takribani 60% ya dawa zote zinazotumika hapa nchini hutumiwa na sekta ya wanyama (mifugo na Uvuvi) ambapo mlaji wa mwisho ni Binadamu kwahiyo kaeni tengenezi mikakati ya pamoja kwa kushirikina na jamii, mje na mkakati utakaosaidia kulimaliza tatizo hili.” Amesema Waziri Ulega
Aidha, Waziri Ulega ametoa wito kwa wauzaji wa dawa na watengenezaji wa chakula katika kuchochea mapambano ya dawa dhidi ya vimelea sugu vya magonjwa.
Kwa upande wake Prof. Robinson Mdegela kutoka Chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA) wakati akitoa mada amesema tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni changamoto mtambuka na ni vema tuzidishe juhudi katika kupambanna nalo.
“Dunia kote tumekubaliana kuja na dhana ya Afya Moja ili kuunganisha nguvu kupambana na hili, namna ya kupambana ni kufanya tathmini kwa tulipofikia ambapo changamoto utaona ni elimu kwahiyo tuelimishe watu ili wajue na kisha kuliepuka.” Amesema Prof. Mdegela