Na Hellen Mtereko, Mwanza
Watumishi wametakiwa kutumia kwa uamifu fedha za miradi mbalimbali zinazotolewa na Serikali sanjari na kuzipeleka kwenye miradi iliyokusudiwa hatua itakayosaidia maendeleo kupatikana kwa haraka.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Siasa,itikadi na uenezi Paul Makonda wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mleba aliposimama njiani Mkoani Kagera ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika Mikoa ya Kanda ya ziwa.
Makonda amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya mambo mengi hivyo fedha anazozileta katika Wilaya ya Muleba zinatakiwa zitumike vizuri ili kukamilisha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
Aidha katika hatua nyingine Makonda amesema katika Wilaya hiyo kuna harufu ya rushwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Ofisi za utumishi wa umma na Polisi hivyo ataongea na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru ili kuweka timu maalumu itakayoweza kudhibiti rushwa.
Mwisho Makonda akatoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wakati wa kukijenga Chama na kusikiliza kero za wananchi wanyonge, kuwatetea wakulima na wafugaji umefika huku akitoa ahadi kwa wananchi wa Muleba kabla ya kumaliza mkutano Chato ataongea na Waziri wa maji ili amwambie mpango uliopo wa kuhakikisha wanapata maji ya uhakika.