Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali akito taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri katika Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake lililoanza Novemba 7 hadi 10,2023 katika Viwanja vya TGNP Mabibo Dar e salaam – Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali akito taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri katika Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi akielezea kuhusu yaliyojiri katika Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake
****
👉Waibua Ongezeko la visa vya madhara yanayotokana na changamoto za afya ya akili
👉Wimbi kubwa la ukatili na unyanyasaji wa watoto wa kiume
👉Wimbi la mikopo kausha damu
👉Kushika kasi kwa wizi na ulaghai wa mitandaoni
👉Wataka Mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya umaliziwe
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Wanaharakati wa haki za wanawake walioshiriki wa Tamasha la 15 na Jinsia na Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake wametambua na kuchambua changamoto zilizopo kwenye jamii zao na kuibua masuala mbalimbali ikiwemo kuibuka kwa wimbi kubwa la ukatili na unyanyasaji wa watoto wa kiume ambapo wameshauri iwe ni moja ya ajenda kuu ya mapambano.
Akito taarifa kuhusu yaliyojiri katika Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake lililoanza Novemba 7 hadi 10,2023 katika Viwanja vya TGNP Mabibo Dar e salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Gemma Akilimali, amesema washiriki wamebaini uwepo wa ukinzani kati ya baadhi ya sera, sheria, mila, desturi na tamaduni ya baadhi ya jamii.
Kuhusu Masuala ya Kisera na Kisheria, amesema Washiriki wamesisitiza umuhimu wa kumalizia Mchakato wa Katiba ambao ulikuwa na madai 11/12 ya wanawake ambayo yalilenga kuboresha ushiriki wa wanawake katika kuleta maendelea ya nchi.
“Jambo jingine lililoibuliwa ni umuhimu wa kuendelea kuchechemua mabadiliko ya kimfumo ambayo inaingilia na kuchelewesha upatikanaji wa haki hususani haki za wanawake, wasichana na watoto. Mfano hadi sasa Mswada wa marekebisho ya sheria ya ndoa ili kubadilisha umri wa chini wa kuoa au kuolewa haujaenda bungeni”,amesema Bi. Akilimali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali
Amesema pia kuna upungufu wa rasilimali fedha za kuendeleza shughuli za kupiga vita mifumo kandamizi na ya kinyonyaji inayofanya baadhi ya makundi kukosa haki zao za msingi na za kikatiba na uwepo wa ukinzani kati ya baadhi ya matamko ya sera na miongozo ya utekelezaji wa sera hususasi katika baadhi ya sekta za huduma za kijamii mfano, suala la utolewaji wa huduma za afya kwa akimama wajawazito bila malipo.
Hali kadhalika , wameibua suala la uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika sekta ya kilimo kushindwa kuangalia jinsi mkulima mdogo na maskini anavyoshindwa hata kugharamia pembejeo licha ya kuwepo kwa ruzuku za serikali na hivyo kulazimika hata kuuza baadhi ya rasilimali alizonazo ili aweze kumudu kulipia gharama za pembejeo na kuishia kulima sehemu ndogo sana.
Kwa upande wa Masuala ya Kijamii mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na uendelevu wa mfumo dume ndani ya jamii na ndani ya taasisi mbalimbali, pia hakuna majukwaa ya kutosha ya wakulima hasa wakulima wanawake ambao wanazalisha mazao ya chakula kupaza sauti zao.
Amesema wanaharakati hao wameibua changamoto ya Mikopo Umiza ambapo kushika kasi kwa wimbi la mikopo kausha damu inaathiri zaidi uchumi wa wanawake na watu maskini.
“Aidha kuna changamoto ya kushika kasi kwa wizi na ulaghai wa mitandaoni ambao unaathiri sana wanawake na wazee pamoja na kukosekana kwa elimu inayofungamanisha matumizi ya TEHAMA na ubunifu kwa wajasiriamali wadogo na wakulima”,amesema.
“Changamoto nyingine ni elimu ya haki za kikatiba na kisheria bado haijawafikia wanawake wengi walioko vijijini na maeneo mengi ya pembezoni mfano ni elimu ya haki sawa ya umiliki wa ardhi na ridhaa ya wanandoa wote wawili wakati wa kuuza mali ya familia”,amefafanua.
Katika Tamasha hilo, changamoto nyingine iliyoibuliwa ni Mabadiliko ya tabia nchi pamoja na matumizi makubwa ya mbolea na viatilifu vya viwandani pamoja na uchafuzi wa mazingira imekuwa ni tishio kubwa kwa upatikanaji wa chakula salama sambamba na jamii kutotoa ushirikiano katika utoaji wa taarifa kwenye masuala ya ukatili kwa kuendekeza mila na desturi kandamizi pamoja na kuongezeka visa vya ukatili majumbani.
Kuhusu Huduma za Kijamii, Wanaharakati wameibua changamoto ya kuendelea kuwepo kwa rushwa katika taasisi za afya hivyo kukandamiza haki msingi za afya kwa wote ambapo kumeonekana kukithiri kwa rushwa ya vitu na fedha.
“Matumizi ya uzazi wa mpango kupungua kwa hofu kubwa juu ya madhara ya njia zilizo haipo za uzazi wa mpango, Ongezeko la visa vya madhara yanayotokana na changamoto za afya ya akili ni changamoto zingine zilizoibuliwa kwenye tamasha la 15 la Jinsia”,ameongeza Akilimali.
Wanaharakati hao pia wamebaini kuwepo kwa Mazingira duni ya elimu kwa watoto wenye ulemavu, hususan kwenye masuala ya vifaa wezeshi.
“Tumebaini pia kukosekana kwa afua za kutosha katika ngazi ya halmashauri zinazojielekeza katika kutatua changamoto za masuala ya afya aya uzazi kwa wasichana mashuleni na nje ya shule mfano elimu juu ya hedhi na usafi binafsi haitolewi kwa kiasi cha kutosha”,ameeleza.
NINI KIFANYIKE?
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TGNP amesema Washiriki wa Tamasha la 15 la Jinsia wamependekeza Mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya umaliziwe.
Aidha wameshauri na kupendekeza Serikali kuboresha mfumo na utaratibu wa utoaji wa mikopo yHalmashauri na mafunzo ya uendeshaji miradi/biashara na utunzaji wa fedha kwa wanawake, vijana na makundi mengine ili kupunguza urasimu na kuwezesha upatikanaji rahisi wa taarifa kuhusu fursa kwa makundi hayo.
“Tumependekeza Halmashauri ya Wilaya, hususani, maafisa biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kuwapatia taarifa (kupitia teknolojia ya simu) na kuwajengea uwezo wanawake na makundi mengine ya pembezoni wanaoshiriki katika kilimo kutambua na kufikia masoko na kunufaika na bei nzuri kwa mazao yao”,amesema Akilimali.
Pia wamependekeza Wajumbe wa Kamati za Vijiji kuweka hamasa na kutumia fursa mbalimbali za kujiongezea uwezo na uelewa kuhusu elimu ya afya ya uzazi ili kuwa mstari wa mbale katika kusimamia kwa ufanisi wa utoaji huduma hizo.
Mapendekezo mengine ni Serikali za Vijiji kwa kupitia Utaratibu uliowekwa na TAMISEMI wa Fursa na Vikwazo vya Maendeleo (yaani O&0D) kutambua na kuweka kuwa kipaumbele upatikanaji wa vifaa tiba na idadi ya kutosha ya watoa huduma kwenye zahanati na vituo vya afya.
Pendekezo jingine ni kuchagiza mapitio na marekebisho ya sheria (Uchaguzi Serikali za Mitaa) na Kanuni ili kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake na makundi mengine kujumuishwa na kushiriki kikamilifu kugombea nafasi za uongozi na vyombo va maamuzi katika ngazi mbalimbali.
Aidha wamependekeza kuhamasisha vikundi vya kijamii (wanawake, wanaume, vijana, wazee, watu wenye ulemavu) na Viongozi wa mila na dini ili kuwa mstari wa mbele kutoa elimu na kuongeza uelewa kwenye jamii kuhusu haki za wajane kurithi na kukemea ukatili na dhuluma za ndoa za utotoni na ukeketaji.
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi akielezea kuhusu yaliyojiri katika Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi amesema Tamasha la Jinsia ni muendelezo wa mkakati wa taasisi tangu mwaka 1996 kuunganisha sauti ya pamoja na kutekeleza mikakati ya kufikia usawa wa kijinsia.
Amesema Tamasha la Jinsia limekuwa sehemu ya kuendelea kutanua harakati za ujenzi wa nguvu za pamoja nchini na kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki.
Liundi ameeleza kuwa, ili kukomesha ukatili wa kijinsia ni lazima kufanyike uchambuzi wa kina kwenye makundi ya jamii kwani kubaini kiini cha tatizo ndiyo suluhu mtambuka huku akisisitiza umuhimu wa kuzuia ukatili kabla haujatokea.
Katika hatua nyingine washiriki wa Tamasha hilo wameandaa mikakati ya utekekelezaji wa mapendekezo yaliyoibuliwa kutoka kwenye warsha kwa kuzingatia hali halisi kwenye kanda, rasilimali zinazowazunguka na kwa kupitia nguvu za pamoja ambapo kwa namna ya kipekee, mikakati hiyo imetambua umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa mila, dini na wa Serikali katika ngazi ya vijiji kata na Halmashauri.
KUHUSU TAMASHA LA 15 LA JINSIA NA MIAKA 30 YA TGNP NA TAPO LA UKOMBOZI WA WANAWAKE
Mgeni Rasmi wa Tamasha la Jinsia alikuwa ni Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka, ambaye alikuwa ni Makamu wa Rais Afrika Kusini (Mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo) na pia alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UN Women Duniani ambaye ameipongeza TGNP kwa kuongoza harakati za kuleta usawa wa kijinsia nchini kupitia ujenzi wa nguvu za pamoja.
Tamasha la 15 la Jinsia limeongozwa na mada kuu isemayo, “Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake” huku mada ndogo ndogo zikiangazia Miaka 30 ya TGNP na Tapo la ukombozi wa wanawake, nyayo zetu urithi wetu, simulizi za mabadiliko, changamoto na mikakati, Miaka 30+ ya tapo la ukombozi wa wanawake –dira yetu, ndoto zetu.
Tamasha la 15 la Jinsia limekutanisha zaidi ya washiriki 2000 wanaojumuisha wadau wa maendeleo (Ubalozi za Uswidi, Ubalozi wa Canada, Global Affairs Canada, Ireland, Nertherlands, Chuo cha Coady International, Shirika la UN Women, UNFPA, Women Fund Tanzania, SeedChange, Crossroads International, Aga Khan Foundation, ), Serikali ya Jamhuri ya Tanzania ambayo imeshiriki kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, na Halmashauri mbalimbali sekta binafsi, asasi za kiraia, vikundi vya kijamii na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega na TGNP katika kuchagiza usawa wa jinsia nchini nan je ya nchini.