Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge ameiagiza Halmashauri ya Kisarawe kuhakikisha ujenzi wa mradi wa shule ya Sekondari ya Kitanga iliyopo kata ya Msimbu unakamilika kabla ya Novemba 23 mwaka huu.
Aidha ameelekeza kufikishwa kwa nishati ya umeme katika shule hiyo ifikapo 15 Disemba , huduma ambayo itanufaisha shule pamoja na wananchi wa eneo hilo.
Akitoa maagizo hayo wakati akikagua mradi wa shule ya Sekondari Kitanga, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani humo, Kunenge alieleza kukamilika haraka kwa ujenzi huo ,itasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kufuata huduma ya elimu umbali mrefu,ambapo kwasasa wanatembea umbali kuanzia km 6-16.
Alieleza, hali hiyo inaumiza , hivyo halmashauri ihakikishe ujenzi unakamilika haraka ndani ya muda huo.
Pia ameuelekeza Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA)kuangalia namna ya kufikisha maji shuleni hapo ili wanafunzi wapate maji safi na salama.
Pamoja na hayo alitoa wito kwa wazazi kuwapa fursa watoto wa kike ya kupata elimu.
“Ninasisitiza elimu kwa watoto wa kike izingatiwe kama tunataka 50 kwa 50 ni lazima watoto wa kike wasomeshwe, kutokana na hilo ndio maana Rais wetu dkt Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kujengwa shule na mabweni kwa ajili ya watoto wa kike” alisema Kunenge.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Fatma Nyangasa alifafanua , kata ya Msimbu ilikuwa na Shule moja ya Sekondari hali ambayo ilisababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya Sekondari.
Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alitembelea ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA) Kazimzumbwi, alikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri , sanjali na kuongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara .