Mwenyekiti wa bodi ya REA Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amewapongeza Wakala wa nishati Vijijini kwa kazi wanayoifanya katika kuhakikisha umeme umeenea kwenye vijiji mbalimbali na kueleza kuwa jambo hilo linasaidia wadau wa maendeleo kuendelea kuongeza nguvu zaidi kuchangia.
Amezungumza hayo wilayani Babati mkoani Manyara wakiwa kwenye ziara ya REA na Wabia wa Maendeleo kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini.
Akiwa kwenye eneo la mwekezaji anayezalisha Umeme Kilowati 320 na kuiuzia TANESCO kwenye maporomoko madogo ya Darakuta Haydropower, Balozi Kingu amepongeza jitihada hizo ambazo zinasaidia serikali kuendelea kuwa na Umeme wa Uhakika.
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka wakala wa Nishati Vijijini Avera Mwijage, amesema katika juhudi za serikali kupitia wizara kuhakikisha miradi ya kufua Umeme iliyo chini ya wawekezaji inaendelea kufanya kazi vizuri na kuwa endelevu, inaihimiza TANESCO kuwalipa waenezaji hao kwa wakati hasa wale wanaouza umeme moja kwa moja kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema limekuwa ni suala wanalolisimamia kwa karibu kwa kutambua kuwa miradi hiyo haina chanzo kingine chochote cha fedha ili kujiendisha kulipa watumishi lakini pia kuhakikisha matengenezo yanafanyika kwa wakati ili taifa liendelee kunufaika na umeme kutoka kwenye vyanzo hivyo.
Naye Mkurugenzi wa Darakuta Haydropower Ritha Batsi ameiomba serikali kusimamia wananchi wanaoishi pembezoni mwa mlima Magara wilaya ya Mbulu kuacha kufanya shughuli zinazoathiri mto huo unaotiririsha maji waliyoyatega kwa ajili ya uzalishaji Umeme.
Akizungumza kwa niaba ya wabia wa Maendeleo, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania Steven Motifamba, amesema kutokana na matokeo mazuri yanayoonekana ikiwa pamoja na usimamizi mzuri wa matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na wadau, wapo tayari kuendelea kuchangia zaidi ili wananchi waendelee kufurahia nishati ya Umeme na Maji kwa maendeleo.
Wadau wa Maendeleo wanaoisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya Umeme Vijijini na Maji ni pamoja na Sweden, Umoja wa Ulaya,Benki ya Dunia, Benki ya maendelo ya Afrika, Norway na Uingereza.