Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga akimkabidhi simu janja na jokofu mshindi wa jumla, Paschal Saba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Novemba 8, 2023 katika viwanja vya Bombadia mjini Singida. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Singida, Alphonsina James, Meneja wa NMB Mkoa wa Singida, Emmanuel Kishosha na Meneja wa NMB, Kanda ya Kati, Janeth Shango.
…………………………………………………………….
Na Dotto Mwaibale, Singida
BENKI ya NMB imezindua kampeni ijulikanayo Teleza
Kidijitali- Weka na Ushinde ambayo inalenga kuchagiza wateja wa benki hiyo
kujenga utamaduni wa kuweka fedha na akiba kwenye akaunti zao.
Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango akizungumza
katika awamu ya pili ya uzinduzi wa kampeni hiyo kitaifa uliofanyika mkoani
hapa Novemba 8, 2023 alisema benki hiyo imekuja na kampeni hiyo baada ya
kutambua kuwa uwekaji wa akiba kwa watanzania imekuwa jambo gumu hali
inayosababisha panapotokea jambo linalohitaji fedha wanalazimika kutafuta
mikopo ya haraka ambayo inakuwa na riba kubwa.
“Suala la uwekaji wa akiba linazidi kuwa
kubwa na sisi kama benki ya NMB inayowajali wateja wake tumeona tuje na kampeni
hii ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kusaidia idadi kubwa ya wateja
wetu kuwa na tabia ya kujiwekea akiba ili wasipate wakati mgumu wanapokumbana
na masuala yenye udharura,” alisema Shango.
Shango alisema kupitia kampeni hiyo Benki ya NMB
inaendelea kuhamasisha wateja wake kutotumia akaunti zao kama sehemu tu ya
kufanya miamala na kupitisha pesa bali wazitumie vyema kujiwekea akiba na
kuhifadhia pesa kwani kufanya hivyo watanufaika baadae.
” Ili kurudisha faida tunayoipata kama benki
kwa wateja wetu tumezindua promosheni hii itakayoshuhudia zawadi ya pesa
taslimu ambayo itawekwa katika akaunti zao ili kuwahamasisha kuendelea kuwa na
akiba katika aaaakaunti zao,” alisema.
Kwa mujibu wa Shango alisema kampeni hiyo itakuwa
na droo za kila wiki na utaratibu wa zawadi utakuwa ni kuongeza kiasi kilichopo
kwenye akaunti yako kwa mara mbili kwa mshindi.
“Ni kwamba kama mteja atakuwa na Sh.Milioni
1 kwenye akaunti yake na ameibuka mshindi, basi sisi NMB tutamuongezea shilingi
milioni moja nyingine, tofauti na kampeni iliyopita kampeni hii tumeamua kuwa
na zawadi ya aina hii ili kuhamasisha zaidi kutumia akaunti za NMB kwa ajili ya
uwekaji wa akiba.
Aliongeza kuwa kampeni hii ambayo imeanza Novemba
8, 2023 itaendelea mpaka wiki ya mwezi Disemba na ni mahususi kwa wateja wote
wa NMB kwa akaunti za akiba na zile za matumizi ambazo ndio za kawaida na hata
kwa wale watakao jiunga na benki hiyo
katika kipindi cha kampeni hii.
“Sisi kama NMB tutaendelea kuhamasisha
matumizi ya akaunti za NMB kama njia ya kuhifadhi fedha na kujiwekea akiba ili
kupata nafasi ya kushinda zawadi hizo na hivyo kufanya kipindi cha kuelekea
mwisho wa mwaka kuwa chenye manufaa zaidi,” alisema Shango.
Alisema Benki ya NMB inazohuduma bora za
kidigitali ambazo zinamanufaa kwa mteja ambazo ni huduma ya mshiko faster
ambayo mteja anaweza kujipatia mkopo mpaka Sh.500,000 papo hapo bila kufika
kwenye tawi la benki kuweka dhamana yoyote.
Alitaja huduma nyingine inayotolewa na benki hiyo
ni ya ;Spend to Save’ ambayo inamuwezesha mteja kuweka akiba kwa kila tumizi
lake kwenye akaunti yake na huduma ya NMB Pesa Akaunti ambayo mteja anaweza
kufungua mpaka kwa Sh.1000 na tayari anakuwa na vigezo ya kujipatia huduma
zingine zinazotolewa na benki hiyo.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma
Mganga akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter
Serukamba, aliishukuru Benki ya NMB kwa kuja na kampeni hiyo ambayo itatoa
elimu kwa wananchi wakipata fedha zao zitakuwa salama na kuzalisha zaidi na
hivyo kuchangia maendeleo ya mkoa huo.
Úwekaje wa fedha kwenye akaunti za NMB ni jambo
jema na linapaswa kupokelewa kwa mikono miwili na kama unafikiri kuweka akiba
sio ujanja basi kutokuweka akiba ukipatwa na tatizo utaona mziki wake na ndio
utajua umuhimu wa kuweka akiba,” alisema Dkt.Mganga.
Alisema suala la uwekaji akiba ni la muhimu sana
katika maisha yetu kwani mara nyingi yamekuwa yakiibuka mambo ya dharura
yanayohitaji fedha na unapokuwa huna akiba utaona ugumu wa kutatua tatizo
husika.
Katika uzinduzi huo Benki ya NMB ilitoa zawadi
mbalimbali kwa washindi wenye akaunti kwenye benki hiyo ambapo mshindi namba
moja Pascal Saba alizawadiwa jokofu kubwa na simu janja huku mshindi namba
mbili akizawadiwa simu.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgoma Lake Ltd, Martin Mtinda alikabidhiwa
trekta la mkopo kutoka benki hiyo lenye
thamani ya Sh.Milioni 27.
Alisema gharama za trkta hilo benki ya NMB
imelipa asilimia 80 na mkulima atalipa asilimia 20 katika kipindi cha miaka
mitatu.
Alisema alipata mkopo huo baada ya kampuni hiyo
kutimiza vigezo kwa kufungua akaunti katika benki hiyo.
Kampeni hiyo ambayo imeonesha kuzaa matunda
itafanyika nchi nzima kwa kuwashirikisha wateja wenye akaunti katika benki hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga akimkabidhi simu janja mshindi wa pili.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga akisoma hutuba ya uzinduzi wa kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
|
Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
|
Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango akiteta jambo na Meneja wa benki hiyo Mkoa wa Singida, Emmanuel Kishosha wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
|
Meneja Masoko wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Ungandeka Mwakatage, akiongoza uzinduzi huo.
|
Uzinduzi ukiendelea. |
Uzinduzi ukiendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga akimkabidhi ufunguo wa triketa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgoma Lake Ltd, Martin Mtinda aliyepewa mkopo na benki hiyo.