Wazriri wa Afya Zanzibar akizungumza na watendaji wa Hospitali ya Najing ya nchini China kuhusiana na zoezi la uchunguzi WA shingo ya kizazi dhidi ya ugonjwa WA saratani ya shingo hiyo huko Hospital ya Mnazimmoja Mjini Unguja.
Na Fauzia Mussa, Maelezo
WIZARA ya Afya Zanzibar kupitia Kitengo cha Maradhi yasiombukiza kwa kushirikina na Serikali ya China jimbo la Jiangsu wanaendelea na kambi ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi katika Hospitali ya Mnazi mmoja.
Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui amesema katika kuimarisha Afya za Wananchi zoezi hilo litaendelea kufanyika kwa lengo la kutatua changamoto hiyo kwa akinamama Nchini.
Alifahamisha kuwa zoezi hilo lina lengo la kuangalia usalama wa shingo ya kizazi dhidi ya ugonjwa wa saratani na kutoa matibabu Kwa wale wote watakaobainika kuwa na ugonjwa huo ndani na nje ya Nchi bila malipo .
“utaratibu wa kuwapatia matibabu umeshaandaliwa hapa nchini, vifaa pamoja na dawa zipo za kutosha kwa ajili ya hayo, na ambao watatakiwa kupata matibabu zaidi nje ya nchi watatibiwa bila ya malipo yoyote.” Alisisitiza Waziri huyo
Aidha Aliwataka Wanawake wote waliofikia umri wa miaka 18 hadi 69 ambao wameshiriki tendo la ndoa kufika Hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi huo ili kuweza kujitambua kama wana viashiria au ugonjwa huo na kupatiwa matibabu mapema .
Kwa upande wake Meneja wa maradhi yasiombukiza Zanzibar Dkt Omar Mohamed Suleiman alisema zoezi kama hilo linatarajiwa kusogezwa Kwa jamii Kwa kuwafikia akina mama katika maeneo mbalimbali ikiwemo vikosi vya SMZ na SMT pamoja na baadhi ya Vyuo vikuu hivyo aliwataka akina mama hao kuitumia vyema fursa hiyo pale itakapowafikia.
Alifahamisha kuwa saratani ya shingo ya kizazi ni moja ya saratani inayoongoza kuwaathiri kinamama Duniani kote ikifuatiwa na saratani ya matiti .
“takribani akinamama laki mbili saabini na tano wanaugua saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka ambapo kwa Zanzibar bado hakuna takwimu sahihi juu ya ugonjwa huo, hivyo zoezi hilo litasaidia kutoa matokeo na kujua hali halisi ya ugonjwa huo ndani ya Zanzibar.”alifahamisha daktari huyo.
Nae Mkurugenzi wa magonjwa ya Saratani kutoka Hospitali ya Najing ya nchini China Dkt Huaijun Zhou alisema katika zoezi hilo wanatarajia kuwafanyia uchunguzi wanawake wapatao elfu tano.
Alifahamisha kuwa zoezi hilo ni muendelezo ambapo kwa awamu nne zilizopita waliweza kuwafanyia uchunguzi wanawake 16,500 ambapo kati yao 840 waligundilika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi kwa hatua ya awali na jumla ya wanawake 90 walibainika kuwa na saratani katika hatua kubwa.
Zoezi hilo linaloendeshwa na wataalamu wa hapa nchini kwa kushirikiana na madaktari kutoka China ni la tano kufanyika Visiwani Zanzibar.