Matenki ya plastiki yaliyotumika kwenye mradi wa maji wa Mlela wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ambao unawanufaisha zaidi ya wakazi 6,200 wa kijiji cha Mlela.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Mhandisi Sudi Dibwine,akionyesha matenki ya plastiki yaliyotumika kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Mlela wilayani humo ambayo yamesaidia kupunguza gharama ya fedha na muda wa utekelezaji wa mradi huo,kushoto mhandisi wa maji wilaya ya Kigoma Aron Kaje
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mlela wilayani Uvinza wakichota maji kwa ajili ya matumizi yao katika kituo cha kuchota maji kilichojengwa kupitia mradi wa maji wa Mlela uliogharimu zaidi ya Sh.milioni 896.
Na Muhidin Amri,Uvinza
ZAIDI ya wakazi 6,200 wa kijiji cha Mlela wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, wameondokana na adha ya kukosa huduma ya maji safi na salama baada ya mradi wa maji wa Mlela-Kandaga kukamilika.
Mradi huo umetekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya Shilingi milioni 896,fedha zilizowezesha kuondoa changamoto kwa wananchi wa kijiji hicho kutembea umbali wa kilomita 2 kila siku kwenda kufuata maji kwenye mito na visima visima vya asili.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Chunya Sudi Dibwine alisema, Sh.milioni 495 ni fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19,Sh.milioni 36 za mfuko wa Taifa wa maji na Sh.milioni 365 zimetokana na mpango wa lipa kwa matokeo(P4R).
Alitaja chanzo cha mradi ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 380 kwa saa, ambayo yanatosheleza kabisa mahitaji ya wananchi wote wa kijiji hicho na kijiji jirani cha Kandaga.
Dibwine alisema,katika ujenzi wa mradi huo wametumia matenki ya plastiki ambayo yamesaidia kupunguza gharama za fedha na muda wa utekelezaji wake, badala ya kujenga matenki ya zege ambayo yangechukua muda mrefu kukamilika na fedha nyingi.
Aidha alisema,katika mradi huo wamejenga jumla ya vituo 15 vya kuchotea maji na wananchi 110 wamevuta maji majumbani,hivyo kuondokana na kero ya kugombea maji na kutumia muda mrefu kwenye vituo vya kuchotea maji.
Kwa mujibu wa Dibinwe,wananchi wa kijiji cha Mlela hawakuwa na huduma ya maji,hivyo mradi huo ni mkombozi mkubwa na umewapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma ya maji.
“mradi huu umetusaidia hata sisi Ruwasa kutimiza malengo yetu ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi umbali usiozidi mita 400,tunamshukuru sana Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan kutupatia fedha zilizowezesha kumtua mama ndoo kichwani”alisema Dibwine.
Dibwine,amempongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa kuwasimamia na kuwaongoza wataalam wa Ruwasa katika kutekeleza miradi ya maji na wananchi wa kijiji hicho kukubali kutoa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo
Katibu wa chombo cha watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) Ulimwengu Shaban alisema,kabla ya mradi huo wananchi walitumia maji kutoka vyanzo vingine ambavyo maji yake hayakuwa safi na salama na hivyo kupelekea kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo ya matumbo.
Ulimwengu alisema,kuanzishwa kwa CBWSO hiyo ni msaada mkubwa kwa serikali kwani jukumu la chombo hicho ni kusimamia mradi,kupeleka huduma ya maji kwa wananchi na kukusanya fedha zinazotokana na mauzo ya maji.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kata ya Mlela Dominic Lombilo,amewapongeza wataalam wa Ruwasa wilaya ya Uvinza na mkoa wa Kigoma kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama hicho.
Hata hivyo amewataka wataalam wa Ruwasa, kuongeza kasi katika kutafuta na kuibua vyanzo vipya vya maji ambavyo vitasaidia kupanua mtandao wa maji kwenye maeneo mengine ambayo hayajafikiwa na huduma ya maji safi na salama.