Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Misungwi
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Misungwi wakiwa kwenye kikao
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuhatarisha usalama kwa jamii kutokana na tukio la vijana wawili kuchomwa moto na baadhi ya wananchi wakidaiwa kuiba mpunga na kuku lililotokea Oktoba 2023 katika Kijiji cha mwaniko Wilaya ya Misungwi.
Makalla ametoa rai hiyo Jana Novemba 6, 2023 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa kusikiliza na kutatua kero katika Wilaya ya Misungwi.
Amesema Mahakama ndio chombo cha kisheria kinachotoa haki hivyo wananchi wanapokua na jambo wanapaswa kulifikisha kwenye sheria ili lisikilizwe na kupatiwa maamuzi sahihi.
“Kwenye hilo tukio zaidi ya wananchi 35 wamekamatwa kutokana na kujihusisha na tukio hilo la kikatili kwa watu wasiokuwa na hatia hivyo ni vyema jambo linapotokea toeni taarifa kwenye mamlaka husika”, amesema Makalla
Aidha, ameiagiza Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Misungwi kukaa na viongozi wa ngazi zote ili kuweka mikakati itakayosaidia kulinda amani kuanzia kwenye kata,Tarafa, Vijiji na Wilaya kwa ujumla.
Hata hivyo Makalla amewataka wananchi wa Misungwi kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi wa Reli ya Kisasa (SGR)ili waweze kijipatia kipato.