Na Mwamvua Mwinyi,Kibiti
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,Abubakari Kunenge, amemuagiza mkandarasi M/S Trinity Manucturing Services Ltd ,ambae anajenga mradi wa maji Kijiji cha Mjawa, wilayani Kibiti ,kuhakikisha anakamilisha ujenzi huo ifikapo Disemba mwaka huu.
Aidha amemuagiza Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji, Kijiji cha Jaribu Mpakani , Broadway Eng.Co.Ltd kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo kabla ya april 2024.
Akitoa maagizo hayo wakati alipokuwa wilaya ya Kibiti ,kukagua miradi ya maendeleo , Kunenge ameeleza wakandarasi wa maji waende na kasi ya Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan ambae amedhamiria kumtua ndoo mama kichwani .
Alieleza, kiu ya Serikali ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji Safi na salama mijini kwa asilimia 95 na Vijijini asilimia 85 ambapo kwa mkoa wa Pwani umefikia asilimia 86 ya upatikanaji wa maji safi .
Vilevile aliwaelekeza, watendaji na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuunganisha huduma ya maji majumbani ili yawafikie kirahisi .
Sambamba na hayo , Kunenge aliwaasa wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya maji na kutunza ili iwe endelevu.
Awali akitoa taarifa ya mradi ,Kaimu Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA)Juma Ndaro alisema, mradi huo utagharimu milioni 503.6 ambapo hadi sasa mkandarasi ameshalipwa milioni 273.004.
Alifafanua, mradi huo utahudumia wananchi wa Kijiji cha Mjawa 3,113, na umefikia asilimia 80.
Kuhusu mradi wa maji Kijiji cha Jaribu Mpakani na Mtawanya Ndaro alisema, utagharimu sh.milioni 831.3 , mradi ambao utahudumia wananchi zaidi ya 10,000, na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 65.
Baadhi ya wakazi wa Mjawa , walieleza wamekuwa wakichota maji yasiyo salama kwa afya visimani ,umbali wa km 10 Jambo ambalo linawapa kero.
Akitembelea mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Jaribu ambayo imejengwa ili kupunguza changamoto ya wanafunzi wanaotoka Mjawa kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya Sekondari, alielezwa bado inahitajika milioni 210 kukamilisha ujenzi huo.
Kutokana na hitaji hilo, Kunenge alieleza, atazungumza na Katibu Tawala mkoa pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi.
“Ujenzi upo vizuri lakini kunahitajika ushauri wa kitaalamu kutokana na mazingira ya eneo hili kuwa kwenye mteremko,ujenzi unachukua gharama kubwa “
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, alieleza mwaka 2021/2022 halmashauri ilipokea sh.milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ikiwemo madarasa nane, maabara,chumba Cha TEHAMA, matundu ya vyoo na mfumo wa maji na matanki ya maji ambapo ujenzi umefikia asilimia 80.