Mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI) akifanya mazoezi kwa vitendo kwenye mtambo maalum wa kidigitiali wa kunyakulia mizigo (Crane Simulator) chuoni hapo jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa mtambo maalum wa kidigitali wa kunyakulia mizigo (crane simulator) ambao umenunuliwa na Serikali kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kilichopo jijini Dar es Salaam. Mtambo huo umegarimu zaidi ya Shilingi bilioni mbili.
Mkufunzi wa Chuo wa Bahari Dar es Salaam (DMI), Elinathan Blasius akizungumza na waaandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mtambo maalum wa kidigitali (Crane simulator) ulionunuliwa na Serikali kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho jijini Dar es Salaam.
PICHA NA WIZARA YA UCHUKUZI.
……….
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi imetumia zaidi ya shilingi bilioni mbili kununulia mtambo maalum wa kidigitali wa kunyakulia mizigo (Crane Simulator) ili kurahisisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma kozi za uendeshaji mitambo katika wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Chuo cha DMI Dkt. Tumaini Gurumo amesema elimu ya uendeshaji wa mitambo unahitaji wahitimu kufanya mazoezi ya nadharia na vitendo ili kuwezesha kuwa mahiri katika utendaji.
“Kozi za uendeshaji wa mitambo hususani kwenye mitambo ya kunyakua vitu vizito zinahitaji uzoefu kwenye nadharia na vitendo hivyo kupitia mtambo huu wanafunzi watatakiwa kufuzu kwenye maeneo yote ili kuwezesha kufanya kazi kwa weledi, tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita kwa kuwezesha jambo hili” alisema Dkt. Tumaini.
Dkt. Tumaini amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa chuo cha DMI lengo likiwa kuhakikisha chuo hicho kinazalisha wataalam watakaoweza kushindana sokoni lakini pia kuweza kuendesha miradi mikubwa inayotekelezwa nchini hasa miradi ya ujenzi wa meli katika maziwa Nchini.
Kwa upande wake Mkufunzi wa DMI, Elinathan Blasius amesema mtambo huo wa kisasa unaotumia teknolojia ya kompyuta utawawezesha wahitimu kwenda na wakati hasa kwenye upakiaji na upakuaji wa mizigo katika bandari, Viwandani na kwenye migodi.
Kwa upande wake Mwalimu Leonard Mwesiga ametoa rai kwa wanafunzi wanaopenda kujiunga na kozi hiyo kutuma maombi ili kuongeza wataalam kwenye eneo la uendeshaji mitambo.