Tenki la kuhifadhi lita 300,000 za maji lililojengwa kwenye mradi wa maji wa Majimoto- Tupindo-Usevya utakaohudumia zaidi ya wakazi 35,000 wa vijiji vitano vya Halmashauri ya wilaya Mpimbwe mkoani Katavi.
Sehemu ya umeme jua(solar)ambazo zitatumika kuendesha mashine ya kusukuma maji kwenye mradi wa Majimoto-Tupindo-Usevya Halmashauri ya wilaya Mpimbwe mkoani Katavi.
Na Muhidin Amri,
Mlele
ZAIDI ya shilingi bilioni 4 zimetolewa na Serikali ili kujenga mradi wa maji wa Majimoto- Tupindo-Usevya ambao utamaliza kero ya maji safi na salama wakazi 35,000 wa vijiji vitano katika Halmashauri ya wilaya Mpimbwe mkoani Katavi.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mlele Mhandisi Madaha Majagi,amesema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa waandishi wa Habari walioko kwenye ziara ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa matenki mawili ya maji,moja la lita 200,000 na lingine la lita milioni 1,200,000,ujenzi wa ofisi ya jumuiya ya watumia maji(CBWSO) katika kata ya Majimoto na ya Usevya.
Alisema, kazi zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya mlinzi kwenye chanzo na nyingine kwenye mitambo ya umeme jua,ujenzi wa nyumba ya nishati(Pump House) na kufunga umeme jua(solar power)na chanzo mradi ni maji ya mserereko kilichopo kijiji cha Mamba.
Kwa mujibu wake Majagi ni kwamba hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 87 na ifikapo mwezi Disemba 2023,mradi huo utaanza kufanyiwa majaribio.
Aidha alisema,kabla ya mradi huo kulikuwa na miradi midogo midogo katika vijiji hivyo ambapo wananchi walikuwa wanatumia maji ya visima virefu ambavyo maji yake yalikuwa na chumvi,hivyo mradi huo unakwenda kumaliza tatizo hilo kwa wananchi.
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Katavi Peter Ngunula alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023/2024 wanatekeleza miradi 50 katika vijiji mbalimbali ikiwemo mradi wa Majimoto- Tupindo-Usevya.
Kati ya hiyo,miradi 25 imekamilika na miradi 25 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na itakapokamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 70.7 hadi kufikia asilimia 88.
Pia alisema, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Ruwasa mkoa wa Katavi imepangiwa kutumia Sh.bilioni 9 ambazo zinakwenda kutekeleza miradi iliyobaki na miradi mipya ambayo imepangwa kutekelezwa.
Ngunula, ameiomba jamii kuhakikisha inashirikiana na serikali kutunza miradi na miundombinu ya maji,vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla kwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi hiyo.
Mkazi wa kijiji cha Usevya Simon Francis,ameiomba serikali kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa ili waweze kupata maji safi na salama kwani wamechoka kutumia maji ya mito ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Regina Kapembwa alisema,katika kijiji hicho hakuna maji ya bomba badala yake wanatumia maji kutoka vyanzo mbalimbali vya asili ambavyo havitoshelezi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya watu waliopo katika kijiji hicho.