Meneja wa Ruwasa wilaya ya Urambo mkoani Tabora Mapengu Gendei wa nne kushoto na wasimamizi wa ujenzi wa mradi wa bwawa la kuvuna maji ya mvua linalojengwa katika kijiji cha Kalemela A wilayani humo,wakiangali baadhi ya miundombinu itakayotumika kwenye utekelezaji wa mradi huo.
Eneo linaloandaliwa kujengwa kwa bwawa la kuvuna maji ya mvua linalojengwa katika kijiji cha Kalemela A wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Urambo Mhandisi Mapengu Gendei kushoto,akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Kalemela A Marry Mtiliga kulia, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa lakuvuna maji ya mvua linalojengwa katika kijiji hicho.
Na Muhidin Amri,
Urambo
BAADHI ya wananchi wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora,wameiomba Serikali kukamilisha kwa wakati ujenzi wa mradi wa bwawa la kuvuna maji ya mvua unaojengwa katika kijiji cha Kalemela A ili waweze kuondokana na adha kubwa ya huduma ya maji safi na salama.
Aidha wamemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo, kufanya kazi usiku na mchana ili aweze kukamilisha kazi zilizopangwa kutekelezwa kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha ambazo zinaweza kusababisha ujenzi huo kusimama.
Yahaya Marekani alisema mradi huo ukikamilika,utamaliza kero ya maji safi na salama iliyokuwepo kwa muda mrefu ambayo imesababisha baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo kukosa muda wa kufanya kazi zao za maendeleo.
Marry Mtiliga alisema,changamoto ya maji katika wilaya ya Urambo ni kubwa,hivyo mradi huo ukikamilika utapunguza kero ya maji na migogoro kwenye jamii ikiwemo ya ndoa inayotokea pindi wanawake wanapochelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji.
Alisema hata kwenye vituo vichache vinavyotumika kuchota maji kuna foleni kubwa,hivyo wanalazimika kutumia muda mrefu wakisubiri kupata huduma ya maji kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Mtiliga alisema,hali hiyo inasababisha wakati mwingine kutokea vurugu za kugombea maji ambazo kwa watu wazima hawawezi kuhimili,na kuiomba serikali kuharakisha ujenzi wa mradi huo ili kunusuru maisha ya wananchi wa Urambo.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha
Kalemela A Seif Susulu alisema,wananchi wa kijiji hicho wanaamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji na wengine wanatumia kati ya Sh.600 hadi 1,000 kununua maji kwa ndoo ya lita 20.
Diwani wa kata ya Muungano Shadrack Manyunya,ameishukuru serikali kuanza ujenzi wa bwala hilo ambalo litamaliza kabisa changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa kata hiyo na wilaya ya Urambo.
Kwa upande wake meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Urambo Mapengu Gendai alisema,mradi huo ulioanza kutekelezwa mwezi Mei na utakakamilika mwezi Novemba 2024 kwa gharama ya Sh.bilioni 5.958 na muda wa utekelezaji wake ni miezi 12.
Alitaja kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa tuta la urefu wa mita 998.2 na kwenda juu ni mita 7.8 na litakuwa na uwezo wake kukusanya maji takribani lita bilioni 4.6 kwa mwaka.
Alisema,kati ya maji hayo lita bilioni 3.4 zitatumika kwa ajili ya binadamu na maji lita bilioni 1.2 yatabaki kwa ajili ya viumbe hai wengine na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 37.
Alisema,kukamilika kwa mradi huo kutawezesha hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji 17 na wananchi 148,000 ambao ni sawa na nusu ya wakazi wote wa wilaya ya Urambo wanakwenda kunufaika na mradi huo.
Gendai,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za mradi huo na amempongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.