Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo akipokelewa kwa ngoma ya kibati wakati alipofika Kituo cha afya Uzini kwa lengo la kuboresha Huduma za afya katika vituo vya Msingi.
Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo akimpatia maelekezo Daktari dhamana kituo cha Afya Uzini Fatma Seif Sleiman wakati alipotembelea kituo hicho kwa lengo la kuangalia maendeleo na kuimarisha huduma za Afya katika Vituo vya msingi.
Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo akiangalia utendaji kazi wa kituo cha Afya uzini wakati wa Ziara yake yenye lengo la kuimarisha huduma za Afya katika Vituo vya Afya vya msingi.
Ujumbe wa Benki ya Dunia na watendaji wa Wizara ya Afya watembelea Hospital ya Wilaya iliyopo Mwera Pongwe kuangalia upatikanaji wa huduma ambapo wameridhishwa na huduma zinazotolewa katika hospital hiyo.
Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo akizungumza na watendaji wa Wizara ya Afya wakati alipotembea kituo cha Damu Salama huko Sebleni Mjini Unguja.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo wakati alipotembelea kituo cha damu salama Sebleni.
Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo pamoja na Mkurugenzi mkuu Wizara ya Afya dkt. Amour Suleiman wakiteta jambo wakati wakikagua gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) katika Hospitali ya Wilaya Iiliyopo Mwera Pongwe Wilaya ya Magharibi A
Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Juan Pablo pamoja na watendaji wa Wizara ya Afya wakikagua vifa vya kutolea huduma katika Hospitali ya Wilaya Iliyopo Mwera Pongwe Wilaya ya Magharibi A
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Mussa , Maelezo
Wizara ya Afya Zanzibar inakusudia kuimarisha huduma za Afya katika Vituo vya Msingi kupitia mradi wa WORLD BANK ili kusogeza huduma kwa jamii .
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia, Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui amesema Lengo la kuimarisha Vituo hivyo ni kupunguza wimbi la wagonjwa katika Hospitali za rufaa pamoja na kupunguza Masafa marefu kufuata huduma za Afya.
“Mwananchi anatakiwa asitembee zaidi ya kilomita tano apate huduma zote za Afya, hivyo tunataka kuona mtu akienda kituo cha kwanza (dispensary) awe anapata huduma zote kama vile huduma za mama na mtoto ,hii itasaidia kupunguza vifo na msongamano katika Hospitali zetu za rufaa.” alisema Waziri huyo
Alisema kuwa lengo la ziara ya ujumbe huo ni kuangalia Maendeleo ya huduma za Afya na kwa namna gani Fedha zao zitatumika katika kuimarisha huduma za Afya hasa katika vituo vya Msingi.
Awali Waziri huyo alifahamisha kuwa Wizara tayari imeshapokea kiasi cha Dola Milioni 25 kutoka Benki ya Dunia kwa lengo la kuimarisha huduma hizo Nchini.
Hata hivyo alisema Wizara inaendelea kufanyakazi na Wahudumu wa Afya wa kujitolea CHV ili kuona Wananchi wote wanafika katika Vituo vya Afya kwa wakati sahihi na kupata huduma stahiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Salim Slim alifahamisha kuwa kupitia mradi wa World Bank Serikali itaimarisha Vituo 30 vya Msingi Unguja na Pemba katika hali ya usawa ikiwemo majengo na vitendea kazi.
Aidha alifahamisha kuwa malengo ya Serikali kupitia mradi huo ni kuhakikisha wanaimarisha mifumo ya Afya katika ngazi za chini na kufikia dhamira ya kuwa hakuna anaeachwa nyuma katika kupata huduma za Afya, hivyo Wizara itazisimamia Fedha hizo na kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa .
“tukiimarisha mfumo wa chini wa Afya, katikati tayari umeshakua mzuri basi kila Mwananchi atakuwa na uwezo wa kuhudumiwa pale alipo kwa kupata huduma stahiki na kwa wakati”alisema Dkt.Slim
Kufuatia ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Juan Pablo amesema ameridhishwa na jitihada za Serikali za kuhakikisha wanawapatia Wananchi huduma bora.
Alisema huduma za Afya zinazotolewa katika Hospitali za Wilaya ndizo huduma stahiki anazopaswa kupatiwa Mwananchi na kuitaka Wizara ya Afya kuharakisha kuimarisha huduma hizo kwenye Vituo vya Msingi.
Katika ziara hiyo Ujumbe wa Benki ya Dunia uliambatana na watendaji wa Wizara ya Afya na kutembealea kituo cha Afya Uzini, Hospitali ya Wilaya Mwera Pongwe na kituo cha Damu salama Sebleni.