Bandung, Indonesia.
Wataalam wapatao 20 kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake wameanza rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo wa masuala mbalimbali ikiwemo utafiti, usalama wa makaa ya mawe pamoja na madini mengine katika Kituo cha Human Resource Development Center Geology, Minerals nchini Indonesia.
Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa imepita takribani kipindi cha miezi sita tu baada ya kufanyika mazungumzo na makubaliano ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali katika Sekta ya Madini ikiwemo kuwaendeleza watumishi na wataalam mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kumsimamia na kuendeleza rasilimali madini.
Itakumbukwa mnano Mei, 2023 Tanzania kupitia aliyekuwa Waziri wa Madini ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko walijadili kuhusu kuwekeza katika shughuli za uchimbaji na ushirikiano kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya uchimbaji wa madini ya nchini Indonesia inayoitwa Mining Industry Indonesia.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho yalikuwa ni pamoja na fursa za mafunzo ya shughuli za uchimbaji nchini humo ikiwemo usalama migodini.
Katika siku za awali za mafunzo hayo, ilielezwa kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia umekuwepo tangu mwaka 1955 ambapo Serikali ya Indonesia ilishiriki katika ukombozi wa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na hatimaye nchi hiyo kujenga ubalozi wake jijini Dar es Salaam mwaka 1964. Pia, Serikali ya Tanzania ilianzisha ubalozi wake mwaka 2022 katika jiji la Jarkata nchini humo.
Aidha, kama ilivyobainishwa katika Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka Wa Fedha 2023/24, miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuendeleza Madini Muhimu na Mkakati na kuzijengea uwezo taasisi zake ziweze kutekeleza majukumu yake. Hivyo, kufanyika kwa mafunzo hayo kunadhihirisha dhamira ya Wizara kufikia malengo yaliyopangwa.
Aidha, hayo yanajiri ambapo pia mafunzo mengine kwa watumishi na waatalam wa wizara na taasisi zake wanaendelea na mafunzo yanayohusu namna ya kupata mitaji katika miradi ya madini *(Mining Financing) yanayofanyika jijini Arusha.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na kampuni ya ASNL Advisory Limited pamoja na ushirikiano na kampuni za Auramet International LLC na Bankable Tanzania Limited.
Matokeo yanayotarajiwa ni kuwawezesha maafisa wa Wizara ya Madini na taasisi zake kuwa na ujuzi stahiki wa kuchambua, kusimamia na kukagua miradi ya uwekezaji katika sekta na kushauri namna bora ya kiwezesha miradi hiyo kupata mitaji ya kuwekeza ipasavyo.