Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tanganyika Mhandisi Alkam Sabuni akionyesha mitambo ya ya kisasa ya kutibu maji kabla ya kusambazwaji kwa wananchi.
Na Muhidin Amri,
Tanganyika
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira wilaya ya Tanganyika kupitia vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO),imeanza kutumia mitambo maalum ya kutibu maji kwenye miradi inayojengwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama katika maeneo yao.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tanganyika Mhandisi Alkam Sabuni amesema,mitambo hiyo ni ya uhakika na inajiendesha yenyewe(Automatic) na vigumu kukosea juu ya kiwango cha dawa kinachohitajika kuingia kwenye maji kabla ya kwenda kwa watumiaji.
Aidha alisema, mitambo hiyo imerahisisha kazi kwa wasimamizi wa vyombo vya maji ngazi ya jamii ambao walati mwingine walilazimika kupanda juu ya matenki kwenda kuweka dawa kwa ajili ya usalama wa watumiaji wao.
Alitaja miongoni mwa miradi ya maji iliyofungwa mitambo hiyo ni mradi wa maji Vikonge uliotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya Sh.milioni 608 ambao umekamilika na unatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi zaidi ya 8,400 wa kijiji hicho.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo Sabuni alisema,kabla ya kuanzishwa Ruwasa mwaka 2019 wilaya ya Tanganyika ilikuwa asilimia 65,lakini sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji imefikia asilimia 81.
Alieleza kuwa,kati ya watu laki tatu na sabini na tano wa wilaya ya Tanganyika,watu laki tatu na thelathini wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia vituo vya kuchotea maji(DPS).
Kwa mujibu wake,baadhi ya yao wameingiza maji ya bomba ndani ya nyumba zao na hivyo na hivyo kutimiza adhima ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Pia alisema,kuna miradi 8 inayotekelezwa yenye thamani ya Sh.bilioni 7.9 ambayo utekelezaji wake uko hatua mbalimbali na baadhi imeanza kutoa huduma kwa wananchi licha ya kutokamilika kwa asilimia 100.
Alisema ni matarajio ya Ruwasa kuwa,ifikapo mwishoni mwaka huu miradi hiyo itakamilika na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kutoka asilimia 81 hadi kufikia asilimia 86 na hivyo kuvuka lengo la kitaifa la asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini.
Katika hatua nyingine Sabuni alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Ruwasa wilaya ya Tanganyika imepangiwa kutumia Sh.bilioni 4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vinne kati ya vijiji 16 ambavyo havijafikiwa na mtandao wa maji ya bomba.
Alisema,miradi hiyo itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa maji katika wilaya ya Tanganyika kutoka asilimia 86 ya sasa hadi kufikia asilimia 92.
Amewaomba wananchi kuendelea kulinda na kutunza miradi ya maji inayoendeleza kutekelezwa pamoja na kuvuta maji ndani ya nyumba zao badala ya kuendelea kuchota kwenye vituo.
Msimamizi wa CBWSO katika kijiji cha Vikonge wilayani humo Jackson Chuzi alisema,mtambo huo umesaidia kupunguza makosa ya kibinadamu pale anapokesea kwa kuzidisha au kupunguza kiwango cha dawa kinachohitajika.
Mwenyekiti wa kijiji cha Vikonge Joseph Sungura alisema,kabla ya kukamilika kwa mradi wa maji Vikonge kijiji hicho kilikuwa na uhaba mkubwa wa maji hali iliyowalazimu wananchi wa kijiji hicho kutumi maji ya visima vya asili pamoja na wanyama hivyo kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo magonjwa ya tumbo.