Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo akimsikiliza Afisa Habari Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Mwantanga Juma wakati wa mahojiano ya ana kwa ana kuhusiana na mafanikio ya miaka mitatu ya Dkt.Mwinyi katika Wizara yake.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Sabiha Khamis, Maelezo
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe Tabia Maulid Mwita amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza vyema ahadi zake katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
Ameyasema hayo wakati akifanya mahujiano ya ana kwa ana na Maafisa habari kutoka Idara ya Habari Maelezo huko Ofisini kwake Migombani Mjini Unguja.
Waziri huyo alisema mafanikio hayo yanaonekana katika nyanja mbali mbali ikiwemo ndani ya Wizara ya habari.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika Wizara yake ndani ya miaka mitatu ya Uongozi wa Dkt.Mwinyi Mhe.Tabia alisema Wizara imefanikiwa kuleta mabadiliko mbali mbali ya kimuonekano, na kiutendaji, katika sekta zote zilizo chini ya Wizara hiyo.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya Dkt. Mwinyi Wizara imefanikiwa kuanzishwa nembo ya utambulisho wa Idara ya Habari Maelezo, kubadilishwa muonekano wa gazeti la Zanzibra leo, kubadilisha bei ya kuuzia gazeti hilo kutoka 500-1000, pamoja na kufanikiwa kusambaza gazeti kutoka mikoa 11-31 ya Tanzania .
Vile vile alisema Wizara imefanikiwa kuongeza mapato kupitia Sekta ya Tume ya Utangazaji ambapo imekusanya kiasi cha Shilingi Milioni 310 kutoka 150, kubadilisha muonekano wa ZBC,kuboresha vipindi vinavyotangazwa na Shirika hilo pamoja na kutengeneza Studi tano ndani ya jengo hilo kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.
Akizungumzia Sekta ya Vijana katika Wizara hiyo alisema Wizara imefanikiwa Kujenga vituo vya maendeleo ya Vijana Unguja na Pemba, kutoa elimu ya uzalendo na kuwaandaa vijana kuwa viongozi wa baadae pamoja na kutoa mikopo kwa Vijana kupitia Fedha Zilizotengwa na Rais huyo ili kuwaendeleza kiuchumi.
Kwa upande wa sekta ya Utamaduni Mhe Tabia alisema Wizara inaendelea na Mpango wa kuanzisha chuo cha sanaa kitakachowawezesha vijana kujifunza sanaa za muziki na kazi za mikono, kuandaaa tunzo za wasanii wa muziki wa aina zote ili kuwawezesha wasanii kuendelea kufanya kazi hizo kilasiku pamoja na Kuchukua wasanii wazoefu wa kitaifa na kimataifa kutoa mafunzo kwa wasanii wa Zanzibar ili kuwjengea uelewa juu ya dhana ya kuugeuza mziki kuwa biashara.
Akigusia mafanikio katika taasisi ya Michezo amesema Wizara imefanikiwa kuuboresha uwanja wa amani kwa kuufanya kukidhi vigezo vya FIFA na CAF.
Hata hivyo alisema wamefanikiwa kujengwa kiwanja kipya cha michezo eneo la MatumbakuMjini Unguja na kuboresha uwanja wa Gomani Pemba kwa kuufanya kuwa na uwezo wa kutumika kimichezo hadi nyakati za usiku.
Mahojiano hayo ya ana kwa ana kati ya Waziri wa Habari na Maafisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar yalilenga kuzungumzia mafanikio ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kipindi cha Miaka mitatu ya uongozi wake ndani ya Wizara hiyo.