Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya maadili kwa watumishi na viongozi wa halmashauri ya Ngara. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Kanisa katoliki Ruleje wilayani Ngara tarehe 02 Novemba,2023.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Mathias (katikati)akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya maadili kwa viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Kanisa katoliki Ruleje wilayani Ngara tarehe 02 Novemba 2023.
……
Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi amesema kuwa Maadili ni nguzo muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya nchi yoyote duniani.
Kanali Kahabi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa- Mwanza yalifanyika tarehe 02 Novemba,2023 katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Rulenge Wilayani Ngara Mkoani Kagera.
Katika hotuba yake Kanali Mathias alisema kuwa, “Maadili kwa kiongozi na mtumishi wa umma yana umuhimu mkubwa sana katika utawala na maendeleo ya nchi kwani Kiongozi ama mtumishi wa umma anapokuwa na maadili katika utendaji kazi wake, atahakikisha anafanya kazi kwa uaminifu mkubwa na kusimamia vyema rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi na kuieletea serikali maendeleo.”
Kwa mujibu wa Kanali Mathias, kiongozi ama mtumishi wa umma anapokua na maadili anakua na ujasiri wa kusimamia Sheria, Kanuni, na Taratibu za nchi. “Huwezi kuwa na ujasiri wa kusimamia sheria inayokataza mienendo ama tabia isiyofaa kama wewe mwenyewe mwenendo wako sio mzuri lazima nafsi ikusute” alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya Ngara, alitumia fursa hiyo kuwaonya watumishi wenye mienendo isiyofaa kuacha mara moja tabia hizo. “Kuna viongozi na watumishi wenzangu kutoka Ofisi nyeti kabisa mmekua mkianzisha migongano ambayo haina tija unakuta mtumishi hamuheshimu mkuu wake wa kazi huo ni utomvu wa nidhamu sio sahihi kabisa muache mara moja,” alisema
Kanali Mathias alionya tabia ya baadhi ya watumishi kutumia lugha chafu kwa Viongozi. “Tunawaona baadhi yenu kwenye mitandao ya kijamii mnaanzisha mijadala ya hovyo isiyokuwa na tija kuwasema na kutumia lugha chafu dhidi ya Viongozi, muache mara moja huko ni kukosa maadili” alisema.
katika hatua nyingine, Kanali Mathias alitoa rai kwa washiriki hao kuhakikisha kuwa wanaishi yote yanayoelekezwa katika mafunzo hayo. “Ndugu washiriki tunajifahamu sisi tulioko hapa Ngara tunaguswa vipi na mafunzo haya? Jamani tubadilike leo tuna mafunzo haya yakatubadilishe kama hatutaki kubadilika sisi wenyewe basi sheria zitatubadilisha kwa lazima,” alisema
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa Bw, Godson Kweka alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili imefanya mafunzo hayo katika wilaya ya Ngara kutokana na changamoto mbalimbali za kimaadili zinazoikabili Wilaya hiyo.
Bw. Kweka alieleza kuwa kumekua na tabia ya baadhi ya watumishi na viongozi katika Halmashauri hiyo kutoa siri za serikali kinyume na taratibu. “Wapo baadhi ya waheshimiwa mkiwa kwenye vikao vya maamuzi hata kabla kikao hakijaisha taarifa tayari ziko kwenye mitandao ya kijamii jambo hili ni kinyume na taratibu na ni kosa kisheria,” alisema.
Bw. Kweka alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya madiwani wenye tabia ya kuwakataa watumishi katika Halmashauri bila kuwa na sababu yoyote ya msingi. “Unakuta serikali inaleta watumishi ambao ni wataalamu katika nyanja mbalimbali katika Halmashauri lakini Mhe. Diwani unasimama na kusema hatumtaki mtumishi huyu hafai , sote tunafahamu kuwa ipo sheria ya utumishi wa umma ambayo ina taratibu na hatua za kumchukulia mtumishi aliyefanya makosa kwa hiyo kama kuna jambo taratibu za kuwasilisha suala hilo kwenye mamlaka husika zifuatwe.“
Aidha, Bw. Kweka alikemea vikali tabia ya baadhi ya waheshimiwa Madiwani kuingilia shughuli za kiutendaji. “Kumekua na tabia ya baadhi ya waheshimiwa madiwani kwenda kwenye vituo vya kazi anakwenda shuleni ama zahanati anachukua daftari la mahudhurio anachora mstari na kuulizia mtumishi huyu yuko wapi jamani huko ni kuingilia utendaji wa Viongozi waliopo watumishi hao wana wasimamizi wao kwa hiyo kila kiongozi afanye kwa mamlaka ya nafasi yake,” alisema.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na mada kuhusu mgongano wa Maslahi na uwajibikaji wa pamoja.