WANAFUNZI WAPYA TAASISI YA UHASIBU MKOA SINGIDA WATAHADHARISHWA KUTOJIHUSISHA MAPENZI NA WALIMU
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania
(TIA) Kampasi ya Singida, ambaye pia ni Mratibu wa taaluma, Flora Lemnge, akizungumza na wanafunzi wapya
wa kampasi hiyo katika semina elekezi
kwa wanafunzi hao iliyofanyika Oktoba 30, 2023. Kutoka kushoto ni Mlezi wa
Wanafunzi, Asia Hansy, Mshauri wa wanafunzi, Ambwene Kajula, Mratibu wa Mipango
na Dawati la Malalamiko wa taasisi hiyo, Magreth Emmanuel.
…………………………………………………………..
NA DOTTO MWAIBALE, SINGIDA
WANAFUNZI wapya waliochaguliwa kujiunga na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida kwa msimu wa masomo wa 2023/2024 wametakiwa kutojihusisha na uhusiano wa kimapenzi na walimu.
Kaimu Mkurugenzi wa kampasi hiyo ambaye pia ni Mratibu wa taaluma, Flora Lemnge, ameyasema hayo jana Oktoba 30, 2023 katika semina elekezi kwa wanafunzi hao na kueleza kuwa mwanafunzi atakayejihusisha na uhusiano wa kimapenzi kwa lengo la kujaziwa matokeo mazuri kwenye mitihani yake atakuwa amejivua utu wake bure.
Akizungumzia namna ya usahihishaji wa mitihani hiyo, alisema ukusanywa na kusahihishwa sehemu moja na hakuna mwalimu anayesahihisha darasa alilofundisha anapangiwa darasa lingine na kila swali husahihishwa na mwalimu mmoja hivyo mtihani wenye maswali matano husahihishwa na walimu watano tofauti.
“Sasa hivi nasimama kama mama nafasi yangu ya kitaaluma naiacha kwa muda ‘ewe binti usivue nguo zako kisa upate mtihani itakula kwako’ kuna baadhi yenu mmekuja hapa na kuanza kujipangia walimu baada ya kuona anamshara na yupo ‘smati’ atakukula bure kwani mtihani huo ni uleule utashindanishwa na kampasi zingine za TIA na unasahihishwa na walimu wa ndani na wa nje na si vinginevyo,” alisema Lemnge.
Lemnge, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia sheria zote za taasisi hiyo na nchi na kuhudhuria masomo kwani hilo ndilo jambo walilolikusudia wakizingatia kuwa wazazi wao wamekuwa wakitoa fedha nyingi kwa ajili yao.
Alisema lengo la semina hiyo ni kuwafanya wazijue taratibu zote za taasisi hiyo ukizingatia kuwa wanafunzi hao wametoka katika mikoa mbalimbali na kuwa na tabia tofauti.
Naye Mshauri wa wanafunzi katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Ambwene Kajula aliwapongeza wanafunzi kwa kuchagua chuo hicho na akawashuru wazazi kwa jinsi wanavyojitoa kuwasomesha watoto wao.
Alisema baadhi ya mambo yanayofundishwa katika semina hiyo elekezi ni kutaka kuwaonesha wanafunzi hao mazingira watakayokuwa nayo na jinsi ya kuishi na kufikia malengo waliyoyakusudia hivyo watafundishwa mambo ya aina mbalimbali kama miongozo, sheria na kanuni ambazo wanatakiwa kuzifuata wakiwa katika taasisi hiyo.
Aidha, Kajula alisema pia watawakutanisha na wadau kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) watu wa dawati la jinsia, NSSF, NHIF na Taasisi za kifedha kama mabenki,vyombo vya mawasiliano ya simu na kuwafundisha mbinu mbalimbali za kimaendeleo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mipango na Dawati la Malalamiko wa taasisi hiyo, Magreth Emmanuel aliwataka wanafunzi hao wanapokuwa na changamoto mbalimbali kuziwasilisha kwa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho.
“Kunatabia baadhi ya wanafunzi wakipata changamoto wanazipeleka kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, TAKUKURU na maeneo mengine hiyo sio sahihi inatakiwa uanzie chini kwa viongozi wa Serikali ya wanafunzi (TIASO) ambao wakishindwa kutatua tatizo lako wanatuletea sisi viongozi wa chuo,” alisema Emmanuel.
Rais wa Serikali ya wanafunzi (TIASO) wa chuo hicho, Godfrey Mbuya alisema moja ya jukumu lao ni kutatua changamoto mbalimbali za wanafunzi na pale zinapowazidi uwezo wanazipeleka ngazi ya juu.
Mbuya alisema semina hiyo ni ya muhimu sana kwao kutokana na mwingiliano wa wanafunzi kutoka maeneo na makuzi tofauti ikiwa ni pamoja na kuyajua mazingira ya chuo na kufuata sheria kanuni na taratibu za chuo.
Japhet Maximilian mwanafunzi wa Shahada ya kwanza katika Rasilimali Watu na Utawala akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake aliushukuru uongozi mzima wa taasisi hiyo kwa semina hiyo elekezi yenye lengo la kuwajenga na kupata miongozo mbalimbali na kuwa mambo yote waliyoelekezwa ni wajibu wao kuyatekeleza.
Maximilian alitumia nafasi hiyo kumshuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwaongeza bumu na hela ya kujikimu kutoka Sh.8,500 hadi Sh.10,000 ni jambo la kuendelea kumshuru kwa kuwa anataka tuwe na taifa la watu walioelimika.
Baadhi ya mambo wanayotakiwa kuyafanya wakati wakiwa chuoni ni kuzingatia uvaaji wenye staha, utunzaji wa mazingira na vifaa vya chuo, heshima kwa kila mtu, lugha nzuri, kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo michezo na kutojihusisha na vitendo vya wizi na mapenzi ya jinsia moja (ushoga na usagaji)
Kesho Oktoba 31, 2023 wanafunzi hao wataendelea na semina hiyo kwa kukutana na taasisi zingine kama TAKUKURU na za kifedha kwa ajili ya kujifunza jinsi zinavyofanya kazi.
Mshauri wa wanafunzi wa taasisi hiyo, Ambwene Kajula, akizungumza.
Mlezi wa Wanafunzi, Asia Hansy, akizungumza.
Mratibu wa Michezo wa taasisi hiyo, Alen Mwanga, akizungumza.
Waziri wa Sheria na Katiba wa taasisi hiyo,
Nurbeti Kabatanye, akizungumza.
Wanafunzi wakifuatilia mada zilizokuwa
zikitolewa.