Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Magula kata ya Sitalike wilayani Mpanda wakkichota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji(DPS)vilivyojengwa kupitia mradi wa maji Magula uliotekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 545 na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa.
Na Muhidin Amri,
Mpanda
MATUKIO ya wananchi wa kijiji cha Magula kata ya Sitalike wilayani Mpanda mkoani Katavi,kushambuliwa na wanyama wakali wakiwemo Simba na Fisi pindi wanapokwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili kwa sasa yamepatiwa ufumbuzi.
Ni baada ya Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ya bomba uliogharimu kiasi cha Sh.milioni.545 katika kijiji hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji cha Magula walisema,kabla ya kukamilika kwa mradi huo maisha yao yalikuwa hatarini kwa kushambuliwa na wengine kuuawa na wanyama hao pindi wanapokwenda kufuata maji kwenye mto na vyanzo vingine vilivyopo katika hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Jane Jonas alisema,kukamilika kwa mradi huo ni jambo la faraja kwa sababu wameondokana na hatari ya kuendelea kuliwa na wanyama hao na kuishukuru serikali kwa uamuzi wa kuwajengea mradi wa maji ya bomba.
Jackob Rajabu alisema,sasa wananchi wa kijiji hicho wanafuraha na amani kubwa kutokana na huduma ya maji safi na salama kupatikana kila mtaa ,hivyo kutoa furs ana kwao kujikita katika shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji.
Alisema,mradi huo umewasaidia vijana kupata ajira ya kuuza maji kwa baadhi ya watu ambao hawajafikiwa na mtandao wa maji ya bomba na kuhaidi kulinda mradi huo ili uendelee kutoa kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake katibu wa chombo cha watumia maji ngazi jamii(CBWSO) Flora Mwita alisema, chombo hicho kimeanzishwa mwezi Machi mwaka 2023 na makusanyo kwa mwezi ni yanafikia kati ya Sh.milioni 3 hadi 4.
Alitaja faida za kuundwa kwa chombo cha watumia maji ni pamoja na mradi kujiendesha kwa faida baada ya kuajiriwa watumishi wenye ujuzi katika kusimamia miradi ya maji na wenue uwezo wa kufanya matengenezo pale miundombinu inapoharibika.
Pia alisema,kasi ya wananchi kuingiza maji kwenye nyumba zao ni kubwa,hata hivyo inatofautiana kati ya kijiji kimoja na kingine kutokana na mwamko na uwezo wa kifedha kwa wananchi wa kijiji husika.
Amewataka wananchi,kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu na kuvuta maji majumbani mwao ili kuunga mkono kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi Mhandisi Christian Mpena alisema,mradi wa maji Magula umetekelezwa kwa kuwatumia wataalam wa ndani na unahudumia zaidi ya watu 7,800 wa vijiji vitatu vya Magula Idindi na Matandalawe.
Alisema,kupitia mradi huo Ruwasa wilaya ya Mpanda imeunda chombo cha watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) kwa ajili ya kusimamia utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mpena,tangu kuanzishwa kwa chombo hicho huduma ya maji imeimarika na kimekuwa msaada mkubwa hasa pale inapotokea changamoto ya miundombinu kuharibika.