Na.Elimu ya Afya kwa Umma, Mkuranga Pwani.
Watanzania wametakiwa kuweka kipaumbele cha lishe bora kwa vijana balehe ili kuimarisha afya ya akili pamoja na afya ya uzazi katika makuzi yao.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 30, 2023 Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani Mhe.Meja Edward Gowele wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiguza.
“Sote tunajua kwamba, kijana balehe ni kijana mwenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 19 ambapo mwanadamu anakua kwenye hatua ya ukuaji kutoka utotoni kuelekea utu uzima. Kipindi hiki ni fursa adhimu kwa ukuaji na maendeleo ya binadamu baada ya siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya binadamu. Ni kipindi cha mpito katika makuzi ya kimwili, kiakili, kisaikolojia na maendeleo kwa ujumla hivyo ni muhimu kuweka kipaumbele cha lishe bora”amesema.
Mhe. Gowele amesema upungufu wa virutubishi katika kipindi cha rika balehe kwa vijana una athari kubwa kwao hali ambayo huchangiwa na mabadiliko katika miili yao kama ukuaji wa haraka, kupoteza damu wakati wa hedhi kwa wasichana na ulaji duni ambao husababisha upungufu wa virutubishi hasa madini chuma na vitamini B9 ijulikanayo kama asidi ya foliki.
Hali kadhalika Mhe.Gowele amesema kundi la vijana linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo changamoto ya utapiamlo wa lishe pungufu, upungufu wa madini na vitamini pamoja na utapiamlo wa lishe ya kuzidi.
“Kulingana na utafiti mwaka 2019 wa ugonjwa wa malaria na hali ya lishe uliofanyika Nchi nzima kwa kundi la wanafunzi wa umri wa miaka 5 – 19 ulionesha kuwa; asilimia 5.1 ya wanafunzi wana unene uliozidi na kundi la wanafunzi wa miaka kati ya 5 na 9 ndio walioongoza kwa asilimia 6.6, asilimia 11.2 wana ukondefu na asilimia 34.2 walikuwa na upungufu wa wekundu wa damu, kundi la wanafunzi wa kati ya umri wa miaka 15 na 19 ndio liliongoza. Pia utafiti huo ulibainisha kuwa asilimia 42 ya wanafunzi wana kiwango cha chini cha kushughulisha mwili au kutofanya mazoezi (yaani tabia bwete)”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya Neema Joshua amesema mtoto akiwa ana lishe duni hata uwezo wa kutulia darasani unakuwa mdogo.
“kundi kubwa vijana balele ni lile la shuleni hivyo anapokuwa analishe duni uwezo wa kushika masomo darasani unakuwa mdogo na yule wa changamoto ya damu kutokana na lishe duni anakuwa anachoka mapema na lishe si kwa afya tu lishe ni kwa ajili ya usalama wa taifa pia maana ukiwa na vijana wenye lishe bora panakuwa na ufanisi”amesema.
Nao baadhi ya Wanafunzi waliohudhuria katika maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa akiwemo Samia Hassan pamoja na Angela Daniel wamesema kupitia Maadhimisho hayo wamejifunza mambo mbalimbali kuhusu lishe ikiwemo kuimarisha afya ya akili pamoja na kuimarisha afya ya uzazi kwa vijana balehe.
Ikumbukwe kuwa Maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa yamekwenda sambamba na kaulimbiu isemayo” “Lishe Bora kwa Vijana Balehe, Chachu ya Mafanikio Yao”ambapo msisitizo umetolewa kwa Viongozi wote katika sekta zote kwa kushirikiana na wadau pamoja na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanaboresha Lishe ya Vijana balehe kwa kutenga bajeti ya kutekelezaji afua za lishe zinazolenga kuimarisha hali ya lishe kwa vijana balehe mashuleni na wale walio nje ya shule nchini Tanzania ikiwemo;Ulaji wa chakula kilichoongezwa virutubishi shuleni,Kilimo cha mbogamboga, matunda na ufugaji wa wanyama wadogo wadogo,Usindikaji na uhifadhi salama wa chakula,Utaoji wa elimu ya lishe kwa vijana balehe,Kufanya tathmini ya hali ya lishe na Unasihi kwa vijana balehe na Usimamizi wa mwongozo wa utoaji wa huduma ya chakula shuleni.