*Yajikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, yatenga shilingi bilioni 900
*Lengo ni kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula
UWEPO wa chakula cha kutosha ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote kwa kuwa bila ya kuwa na uhakika wa chakula hata usalama wa nchi nao huyumba, hivyo ni vyema kujiwekea mikakati ya kuzalisha chakula cha kutosha/
Katika kudhihirisha umuhimu wa usalama wa chakula nchini, hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani lililofanyika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali ulimbatana na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani pamoja na maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO)
Jukwaa hilo ambalo liliwakutanisha wadau wa kilimo wakiwemo vijana, wakulima, wazalishaji wadogo, watunga sera, wawekezaji katika kilimo na wanasayansi duniani, wote wakiwa na lengo la kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula ili kufikia mustakabali bora wa chakula kwa wote.
Akizungumza katika jukwaa hilo Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka mipango inayolenga kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo 2030.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuhakikisha mipango hiyo inafanikiwa, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili kurahisisha shughuli za kilimo. “Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji.”
Waziri Mkuu alisema licha ya jitihada za kuboresha sekta ya kilimo ambazo zimewekwa ndani za kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha kwamba wanaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi, pia Serikali ameamua kuungana na FAO kupitia Mkurugenzi Mkuu na ameahidi kuiunga mkono mipango hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa alisema katika kuhakikisha Taifa linafanikiwa kwenye utekelezaji wa mpango wake wa kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula, Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza kupanua wigo wa kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga shilingi bilioni 900.
Waziri Mkuu alisema kuwa mbali na maboresho hayo yaliyofanyika katika sekta ya kilimo, pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba, upandaji wa mazao, uvunaji na uhifadhi wa mazao hayo hadi kwenye utafutaji wa masoko kupitia maafisa ugani ambao wapo hadi vijijini.
Alisema Serikali imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa kidigitali lengo likiwa ni kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba na aina ya mazao wanayolima ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma za ugani. “Kilimo ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu. Tunataka tujiridhishe kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula.”
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Dkt. Qu Dongyu alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu, hivyo Shirika lao liko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalam pamoja na kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula.
Aidha, Dkt. Qu Dongyu alisema kuwa Shirika hilo limevutiwa na mradi wa kuwawezesha vijana unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania wa Jenga Kesho Iliyobora “Building Better Tomorrow” (BBT). “FAO tutaunga mkono mradi huu ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza malengo ya kuwainua vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo kama ilivyo moja ya agenda kwenye mkutano wa FAO wa mwaka 2023”.
Mkurugenzi huyo wa FAO amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuboresha mahusiano na mashirika ya kimataifa, ambapo ameahidi kutembelea Tanzania mwaka 2024 kwa ajili ya kujionea maendeleo katika sekta ya kilimo pamoja na kupanua wigo wa majadiliano kati ya Tanzania na Shirika hilo ili kuendelea kuwezesha zaidi sekta ya kilimo na uchumi wa Buluu.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema kwa sasa Serikali inafanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo na miongoni mwa maboresho hayo ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambayo inalenga kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali imeendelea kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo kwani mbali na kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kilimo ni miongoni mwa sekta zinazotoa ajira nyingi, hivyo watakuwa wamejihakikishia ajira.
Licha ya kuhudhiria alimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani na maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), pia Waziri Mkuu alifungua katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia lililofanyika Palazzo Regione Lombardia, Milan nchini Italia pamoja na kutembelea shamba la kisasa la ufugaji wa ng’ombe.
JUKWAA LA BIASHATA TANZANIA NA ITALIA
Oktoba 19, 2023 Waziri Mkuu alifungua kongamano la tatu la Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia, ambapo Mheshimiwa Majaliwa alitoa wito kwa Watanzania walioshiriki katika jukwaa hilo wahakikishe wanatumia vizuri fursa walizozipata kutoka kwenye jukwaa hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wafanyabiashara walioonesha nia ya kuja kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeondoa tozo na urasimu uliokuwepo awali kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara na uwekezaji nchini, hivyo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia waje kuwekeza nchini.
“Msisitizo wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mkakati wa Serikali ni kuwahamasisha wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa mbalimbali nchini waje kuwekeza katika ujenzi na kuzalisha bidhaa hizo nchini ili zipatikane kwa wingi na kwa urahisi.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia jukwaa hilo wafanyabiashara na wawekezaji wengi kutoka nchini Italia wameonesha nia ya kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo,madini, uvuvi, afya, mifugo, viwanda na utalii, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa wizara zinazohusika na masuala ya uwekezaji kuchangamkia fursa hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa na maeneo na mazingira mazuri ya uwekezaji pia ina vivutio vingi vya utalii hivyo, aliwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara, pia Mheshimiwa Majaliwa aliyakaribisha makampuni na mawakala wa utalii waje nchini na kuwekeza katika ujenzi wa hoteli za kitalii katika miji mbalimbali yakiwemo majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, viwanja vya ndege na nishati ya uhakika ili kurahisisha shughuli mbalimbali zikiwemo za uwekezaji.
SHAMBA LA MIFUGO MILAN
Sekta ya Mifugo ni moja ya eneo ambalo Serikali ya awamu ya sita imeweka msisitizo wa kuhakikisha inakuwa ili kuwanufaisha wafugaji nchini kwa kuwafanya kufuga kisasa na kuondokana na ufugaji usio na tija.
Dhamira hii ilimfikisha Mheshimiwa Majaliwa katika moja ya shamba la mifugo mjini Milan nchini Italia ambapo Oktoba 19, 2023 alitembelea shamba la ufugaji wa ng’ombe wa maziwa la Alesandra linaloendeshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektoniki ikiwemo ukamuaji wa maziwa kwa kutumia roboti.
Akiwa katika shamba hilo lenye takribani ng’ombe 500, Mheshimiwa Majaliwa alishuhudia mifumo bora ya ufugaji, ulishaji , unyonyeshaji na ukamuaji wa maziwa, ambapo ng’ombe mmoja anauwezo wa kutoa lita kuanzia 35 hadi 70 kwa siku na kumuwezesha mfugaji kupata tija zaidi.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wafugaji nchini wakubali kubadilika na wafuge kwa kutumia teknolijia ya kisasa ili wanufaike zaidi na shughuli hiyo. “Tubadilike tupate manufaa zaidi, ufugaji ni uchumi, ufugaji ni maisha na ufugaji ni kazi, hivyo tubadili mfumo wa ufugaji wetu kwa ajili ya kujiongezea kipato zaidi.”
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema amefurahishwa na misingi bora ya ufugaji na kwamba utaratibu huo ukitumika nchini utaongeza tija katika sekta ya mifugo.
Alisema aina ya ufugaji inayotumika kwenye shamba hilo kuanzia hatua uandaaji wa malisho, ukamuaji wa maziwa, usafirishaji na utunzaji wa mifugo aliojifunza shambani hapo atakwenda kuufanyia kazi kwa lengo la kuimarisha sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema amefurahishwa na namna ya uendeshaji katika shamba hilo ambalo pia wanafanya kilimo mseto kwa kufuga, kulima malisho ya mifugo na kutumia kinyesi cha ng’ombe kuzalisha nishati ambayo wanaitumia kwa shughuli za shambani na ziada kuuza kwenye gridi ya Taifa.
Alisema jambo jingine lililomfurahisha katika shamba hilo ni namna ambavyo mifugo yao imewekewa hereni za kielektroniki kwa ajili ya utambuzi ambazo zinaiwezesha nchini kujua idadi ya ng’ombe pamoja na maendeleo yake ikiwemo kutambua magonjwa, hivyo atakutana viongozi wa sekta husika ili kuangalia namna bora ya kuboresha ufugaji nchini.
Naye, mfugaji wa ng’ombe kutoka Wami Sokoine, Morogoro, Mainga Ole Kalaita ambaye alitembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza ufugaji bora alisema amepata elimu ya ufugaji bora na atakwenda kuwashauri wafugaji wenzake nchini wabadilike ili waendane na mahitaji ya sasa ya soko ikiwa ni pamoja na kubadili njia za ufugaji. “Hakuna haja ya kuwa na mifugo mingi isiyokuwa na tija, tubadilike tufuge kisasa.”
Ole Kalaita alisema kuwa kuna haja ya wafugaji nchini kukubali mifugo iwekewe hereni kwa ajili ya utambuzi wa aina ya uzao wa ngombe kwani katika masoko ya kimataifa lazima wahoji historia ya mfugo, aliiomba Serikali iendelee kuwaelimisha wafugaji umuhimu wa kuwa na taarifa za mifugo.
Awali, mmiliki wa shamba hilo, Bibi Alessandra Soresina alisema katika shamba hilo wanatumia teknolojia ya uhimilishaji wa mifugo kwa lengo la kuwa na kosafu za mifugo yao. Teknolojia hiyo inawasaidia kuwa na uhakika wa kuwa na muendelezo mzuri wa ng’ombe wanaotoa maziwa kwa wingi. “Wakati mwingine hutumia akili bandia ili kuweza kubaini mbegu za ngombe jike pekee kwa ajili ya uhimilishaji ila njia hii hugharimu fedha nyingi zaidi.”
Alisema ng’ombe wote wanapewa chakula kinachozalishwa shambani hapo kwa kuchanganya mahindi na nyasi zilizohifadhiwa vizuri kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mifugo hiyo inapewa chakula mara tatu kwa siku ambapo ratiba hiyo inaweza kubadilika kulingana na msimu. Kwenye shamba hilo hakuna madume na iwapo ikitokea ng’ombe amezaa ndama dume, ndama hao huuzwa.
Aliongeza kuwa ng’ombe wao wamevalishwa hereni ikiwa ni utambulisho rasmi unaohusisha aina, uzao, asili, utambuzi wa mmiliki na kuwezesha ufuatiliaji wa maendeleo yake ikiwemo kutambua magonjwa, uwezo wa kutoa maziwa pamoja na kujua kama anakula vizuri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa alisema mamlaka yao imefaidika sana kwa kushiriki katika jukwaa hilo kwa sababu sekta zote walizozitangaza zikiwemo za ujenzi, viwanda zimeonesha kufurahiwa na wadau wa uwekezaji, hivyo wamejipanga kupokea wafanyabiashara.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kushiriki katika jukwaa hilo na kwamba ofisi hizo za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia zitatoa ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote waliokuwa tayari kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini.